Mwezi Novemba 2012, Kampuni ya Addax Energy SA ya Uswisi ilishinda zabuni ya sita ya kuingiza mafuta kwa pamoja chini ya utaratibu unaosimamiwa na Kampuni ya uagizaji mafuta kwa Pamoja (PICL). Zabuni hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya mafuta ya Mwezi Desemba 2012 na mwanzoni wa Januari 2013.
Utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja
huzingatia pamoja na mambo mengine viwango vya ubora wa mafuta kama
vinavyoelekezwa na Shirika la Viwango nchini (TBS). Aidha, TBS hukagua
ubora wa mafuta hayo kabla hayajaingia nchini.
Pamoja na aina nyingine za mafuta, Addax
Energy SA ilipaswa kuleta mafuta ya dieseli yenye ujazo wa MT
100,000 sawa na takriban lita 100,000,000 katika zabuni ya sita. Meli ya
AL BURAG iliyobeba mafuta hayo ilitakiwa kufika hapa nchini na kupakua mafuta
kati ya tarehe 17 mpaka 20 Desemba 2012. Hata hivyo, meli hiyo ilifika tarehe
24 Desemba 2012 ikiwa imechelewa kwa siku nne kwa mujibu wa ratiba.
Mafuta hayo yalipimwa na TBS tarehe 26 Desemba 2012 na kugundulika kuwa yako
chini ya viwango vinavyotakiwa kwa Tanzania. Aidha, tarehe hiyo hiyo,
Kampuni binafsi ya Intertek Testing Services iliyoajiriwa na PICL
pamoja na Addax Energy SA ilipima mafuta hayo na
kujiridhisha kuwa yalikuwa chini ya viwango vinavyotakiwa.
Kwa kuzingatia hali hiyo Serikali imechukua hatua zifuatazo:
1. Imeiagiza PICL pamoja na EWURA kwamba mafuta YARUDISHWE yalikotoka,
2. Imeiagiza EWURA ichukuwe hatua stahiki za KISHERIA dhidi ya Kampuni
ya Addax Energy SA,
3. PICL ichukuwe hatua zinazotakiwa dhidi ya Kampuni ya Addax Energy SA
kulingana na MKATABA, na
4. Imeziagiza PICL pamnoja na EWURA kuhakikisha kuwa hali hii haijirudii tena
hapa nchini.
Aidha, Wizara ya Nishati na Madini inapenda
kuwahakikishia wananchi kuwa kutopokelewa kwa mafuta hayo yaliyo chini ya
viwango HAKUTAATHIRI upatikanaji wa mafuta ya dieseli nchini kwa kuwa
kwa sasa kuna mafuta ya kutosha.
Imetolewa na
Katibu Mkuu
Dar es Salaam, Desemba 28, 2012
Dar es Salaam, Desemba 28, 2012
Post a Comment