Kutokana
na mgomo wa madaktari uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi juni 2012.Wizara
iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la madaktari Tanganyika ili
lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao .Idadi ya madaktari wote waliogoma
walikuwa 394, kati yao madaktari 376 walikuwa ni madaktari
walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka hospitali za Muhimbili,
K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St.Francis – Ifakara, Dodoma, Temeke,
Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure. Aidha, Madaktari
waajiriwa(Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo kutoka hospitali ya Rufaa
ya Mbeya.
Baraza lilipitia malalamiko
yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki
katika mgomo huo. Adhabu hizo zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo
kali na kusimamishwa udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile
vile kuna Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo
walifutiwa mashtaka.
MCHANGANUO WA
ADHABU
- Waliofutiwa mashitaka madaktari 49
- Waliopewa onyo madaktari 223
- Waliopewa onyo kali madaktari 66
- Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
- Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria madaktari 4
- Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza madaktari 22
Wizara inakamilisha
taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma kwa Madaktari
wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele ya Baraza la Madaktari.
Wizara pia imeridhia kuwapa Madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa
nyingine ya kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo
kabla ya kuondolewa. Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote waliopewa
adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza
kutumikia adhabu zao.
HITIMISHO
Kwa taarifa hii madaktari
wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa onyo na onyo kali wanatakiwa
kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa
msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili na kuruhusiwa
kuendelea na mafunzo kwa vitendo. Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar)
wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa barua zao
kulingana na Adhabu walizopewa. Barua hizi zitatolewa kuanzia tarehe 2 Januari,
2013.Madaktari wote walio katika mafunzo kwa vitendo wanatakiwa kuanza kazi
katika vituo vyao vya awali ifikapo tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda
utakaoongezwa kwa kipindi kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote
waliopewa adhabu wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo
ilivyotolewa
Nsachris
Mwamwaja
Msemaji
WIZARA YA AFYA NA USTAWI
WA JAMII
27/12/2012
Post a Comment