WARAKA WA MAREKEBISHO
YA KATIBA YA TFF WAPITA
Waraka wa marekebisho ya Katiba ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umepita baada ya kuungwa mkono na theluthi
mbili ya wajumbe wa Mkutano Mkuu waliopiga kura.
Jumla ya wajumbe waliopiga kura kwa njia hiyo
ya waraka ni 103 ambapo 70 wameunga mkono wakati waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni
asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo kupatikana theluthi mbili ya kura
zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.
Kura zilizosema ndiyo kutoka kwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa vyama vya mikoa ni 46, wajumbe kutoka vyama shiriki ni 13 wakati
klabu za Ligi Kuu zilizounga mkono ni kumi na moja.
Kamati ya Utendaji ya TFF inawashukuru wajumbe
wote wa Mkutano Mkuu- kwa waliounga mkono na waliokataa kwa vile walikuwa
wanatekeleza wajibu wao wa kikatiba.
Vipengele vilivyoingizwa ni ‘club licencing’ kama
ilivyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi wa TFF kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Vilevile Kamati ya Utendaji itakutana Desemba
23 mwaka huu kufanya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa
kwa marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia
itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.
Mkutano Mkuu wa TFF ambapo pia utakuwa na
ajenda ya uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24 mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya
TFF, wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya Mkutano Mkuu siku 60
kabla.
MIKOA SITA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI TWFA
Mikoa sita ambayo ni wanachama wa Chama cha
Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) haitashiriki katika uchaguzi wa chama
hicho utakaofanyika Desemba 19 mwaka huu mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya TWFA, wanachama hao
hawatashiriki kwa vile hadi sasa haijapokea taarifa za uchaguzi kwenye vyama
hivyo. Vyama hivyo ni vya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Rukwa, Shinyanga
na Tabora.
Uchaguzi huo utafanyika kwenye hoteli ya
Midland, na wagombea ni Isabela Kapera, Joan Minja na Lina Kessy (Mwenyekiti),
Rose Kissiwa (Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma na Cecilia Mkafum (Katibu Mkuu),
Zena Chande (Mjumbe Mkutano Mkuu wa TFF) na Sophia Charles na Triphonia Temba
wanaowania ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Boniface Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)



Post a Comment