Watu wawili wanashikiliwa na makachero wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi Padre Ambrose Mkenda wa Parokia ya Mpendae visiwani Zanzibar.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, ACP Yusuf Ilembo, amesema Kunaswa kwa watuhumiwa hao, kumefanikiwa baada ya juzi serikali kutuma makachero kutoka Bara kuungana na wenzao wa Zanzibar kufanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika na shambulio hilo la kinyama.
Padre Mkenda alipigwa risasi na watu wasiojulikana siku ya Krismasi, nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni, akitokea kanisani. Alishambuliwa akiwa ndani ya gari lake na kuanguka.
Ilembo alisema polisi itahakikisha wale wote waliohusika watatiwa nguvu na kukabiliana na mkono wa sheria, watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sasa kupisha uchunguzi, wanaendelea kuhojiwa na makachero hao visiwani Zanzibar.
Ingawa uchunguzi wa serikali unaendelea, lakini wadadisi wa mambo ya siasa wanalihusisha tukio hilo na uhasama wa kidini.
Tukio la kushambuliwa kwa padre huyo, linafanana na lile la kumwagiwa tindikali kwa Katibu Mkuu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeshikiliwa kuhusika na tukio la Mufti kumwagiwa tindikali, ambalo kwa namna moja au nyingine, limekuwa likihusishwa na mitazamo tofauti ya kisiasa.