Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa kampuni ya simu za
mkononi ya Zantel Ahmed Seif Mohamed (kushoto ) akikabidhi mfano wa hundi yenye
thamani ya Sh.6,040,000 kwa Mwenyekiti wa chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo nchini (Taswa) Juma Pinto, pembeni ya Mohamed ni Meneja Mwandamizi wa
Mawasiliano na Masoko wa Zantel Awaichi Mawala na Katibu Msaidizi wa Taswa,
George John.
KAMPUNI ya simu za mkononi
ya Zantel imejitokeza kudhamini Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utakaofanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu
Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa
Zantel Ahmed Seif Mohamed, alisema wanajisikia furaha kushirikiana na TASWA
kudhamini mkutano huo wa aina yake.
Alisema Zantel imekuwa na
uhusiano mzuri na wanahabari, hivyo walipoombwa hawakusita kufanya hivyo na wana
matumaini makubwa utakuwa mkutano wenye manufaa.
Alieleza kuwa kampuni yake
baada ya kupata mafanikio katika mashindano ya Epiq Bongo Star Search
iliyomalizika hivi karibuni ni nafasi nyingine ya kuendelea kudhamini matukio
mbalimbali ya michezo na burudani kwa kadri uwezo
utakavyoruhusu.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru Zantel na kusema awali chama hicho kiliomba
udhamini kwa kampuni hiyo kwa lengo la kufanya mkutano Dar es Salaam, lakini
sasa walifikiria ufanyike Bagamoyo, Pwani.
Alisema Zantel wamedhamini
kwa kiasi cha Sh 6,040,000 na kwamba bajeti ya mkutano huo ni Sh milioni 20,
hivyo kuomba wadau wengine wasaidie ili kufanikisha mkutano huo utakaohusisha
zaidi ya waandishi wa habari za michezo 100 ambao ni wanachama wa
TASWA.
“Mkutano huo unatarajiwa
kushirikisha wanachama 100, na pia watakuwepo wadau mbalimbali wa TASWA wakiwemo
waandishi wakongwe wa habari za michezo wambao watapewa nafasi ya kuzungumza
kwenye mkutano huo,” alisema Pinto.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
wa chama hicho, aliwasisitiza wanachama kuendelea kuthibitisha ushiriki wao na
kuwa mwisho wa kufanya hivyo ni kesho alasiri.


Post a Comment