Kamishna wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kuchunguza vitendo vya uhalifu wa kivita nchini Syria.
Pillay ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kupeleka rekodi za ukiukaji wa haki za binadamu kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague.
Barua ya malalamiko na kuomba uchunguzi ufanywe iliwasilishwa na Switzerland na kuungwa mkono na nchi 58.
Baraza la Usalama lenye wanachama 15 ndilo pekee lenye mamlaka ya kupeleka malalamiko hayo katika mahakama ya ICC.
Wakati huohuo, waandishi wawili wameuawa katika mashambulizi wakiwa kazini nchini Syria.
Mwandishi wa Kifaransa alikufa katika eneo la kaskazini mwa mji wa Aleppo na mwingine kutoka kituo cha Televisheni cha Aljazeera aliuawa katika kitongoji cha Basra al-Harir kwenye jimbo la Daraa.