Na Daniel
Mjema
KADA maarufu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Shafii Yatera (40), ameuanza vibaya mwaka
2013 baada ya kusherehekea Mwaka Mpya akiwa Gereza Kuu la Karanga mjini
Moshi.
Yatera alipandishwa
kizimbani juzi mbele ya Hakimu mkazi, Sophia Masati
akikabiliwa na tuhuma za
kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Msasani.
Kada huyo ndiye ambaye
katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 alichuana na Mbunge wa sasa wa Jimbo la Mwanga
ambaye pia ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na kushika nafasi ya
pili.Akimsomea mashtaka yake, Wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Oscar
Ngole alidai kuwa Novemba 1,2012, mshtakiwa alimwingilia kimwili mwanafunzi huyo
wa Kidato cha Nne kinyume cha sheria.
Wakili huyo alidai kuwa
kitendo alichokifanya mtuhumiwa huyo ni kinyume cha kifungu 130 (2) (e) na 131
cha kanuni ya adhabu sura ya 16, adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 30
jela. Hata hivyo kada huyo wa Chadema ambaye ni mkazi wa Pasua mjini Moshi
alikanusha mashtaka hayo lakini upande wa mashtaka ukaiomba mahakama kuzuia
dhamana kwa sababu za kiupelelezi.
Wakili Ngole, alidai
kuwa endapo mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana ataathiri uchunguzi wa kesi hiyo
kwa kile kinachodaiwa amekuwa akimshawishi mwanafunzi huyo kutokutoa ushirikiano
kwa polisi.
Hakimu Masati
anayeisikiliza kesi hiyo alilikubali ombi hilo la upande wa mashtaka na kuamuru
mshtakiwa apelekwe rumande katika Gereza Kuu la Karanga hadi Januari 14, 2013
kesi hiyo itakapotajwa tena.
Post a Comment