Na Deodatus
Balile, Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeongeza
ukusanyaji wa mapato katika bandari ya Dar es Salaam kutoka shilingi bilioni 28
mwezi Novemba hadi shilingi bilioni 50 (dola milioni 18 hadi dola milioni 31)
katika mwezi wa Disemba, kufuatia kusimamishwa kwa muda maofisa 16 wa bandari
wanaotuhumiwa kwa mwenendo usiofaa.
Meli zinapakua
makontena katika bandari ya Dar es Salaam tarehe 29 Disemba, 2012. [Deodatus
Balile/Sabahi]
Maofisa hao wa bandari, wakiwemo wakurugenzi wa
ngazi za juu, walisimamishwa kwa muda mwezi Disemba baada ya Wizara ya
Usafirishaji kuanzisha uchunguzi wa ndani kwa lengo la kutoa mwitikio wa
malalamiko ya wateja kuhusu kucheleweshwa katika bandari hiyo, kwa mujibu wa
Waziri wa Usafirishaji Harrison Mwakyembe.
Maofisa wa bandari wengine wasiopungua sita
walisimamishwa mwezi Agosti. Uchunguzi huo, ambao bado unaendelea, uligundua
kuwa waajiriwa wa bandari walibadilisha mwelekeo wa biashara kutoka katika
bandari kwenda kwa kampuni ndogo za usafirishaji na utoaji mizigo wanazomiliki,
ukiukaji wa moja kwa moja wa mkataba wao wa ajira.
"Wateja wanakimbia bandari yetu kwa sababu ya
ucheleshaji wa kukusudia unaofanywa na waajiriwa wasio na maadili ambao
wanaongeza gharama za kufanya biashara," Mwakyembe aliiambia Sabahi. "Hii ni
kinyume na mikataba yao ya ajira na wana mgongano wa maslahi na mwajiri wao
[serikali]."
Miongoni mwa viongozi wa bandari wa ngazi ya
juu waliosimamishwa ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA Ephraim Mgawe, Mkurugenzi wa
Mipango Florence Nkya, Mkurugenzi wa Uhandisi Bakari Kilo, Mkurugenzi wa Mifumo
ya Utawala Maimuna Mrisho, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Ayub Kamili, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Hamad Koshyuma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Julius
Fuko, na Meneja wa Bandari Cassian Ng'amilo.
Mashtaka rasmi bado hayajatolewa dhidi ya
viongozi waliosimamishwa na bado hawajajibu tuhuma zozote hadharani. Mwakyembe
alisema Bodi ya Wakurugenzi ya TPA itakutana hivi karibuni kutoa uamuzi wa
mwisho kuhusiana na ajira yao.
Kwa kawaida, makampuni ya kupokea na
kusafirisha mizigo hutoza shilingi 640,000 (dola 400) kuondoa kontena lenye futi
20 hadi 40 kutoka bandarini ndani ya siku saba. Makontena ambayo hayajalipiwa
ndani ya muda huo uliyotengwa hutozwa fedha za ziada.
Mwakyembe alisema wateja wanalalamika kwamba
kulipia na kutoa kontena katika bandari ya Dar es Salaam kumekuwa kukichukua
hadi wiki nane, wakati inachukua siku saba tu katika bandari ya Mombasa nchini
Kenya.
Wateja wanataka bidhaa kuondolewa bandarini
katika kipindi kifupi kadri iwezekanavyo, Mwakyembe alisema, na pale ambapo kuna
ucheleweshaji bandari ya Dar es Salaam, wanahamishia mizigo yao katika bandari
nyingine, ambako kunasababisha serikali ya Tanzania kupoteza mapato.
Mwakyembe alisema makampuni binafsi
yanayomilikiwa na viongozi tangu wakati huo yamesimamishwa na biashara imerejea
bandarini, na kuchangia ongezeko la mapato ya Disemba.
Makampuni ya kuagiza na kusafirisha bidhaa nje
yakaribisha marekebisho
Vincent Nyerere, anayemiliki kampuni ya kuagiza
bidhaa, alikubaliana na kusimamishwa kwa viongozi wa bandari, lakini alisema
bado jitihada zaidi zinatakiwa ili kuboresha biashara bandarini, kwa kuwa bado
inaenda taratibu.
Alisema aliagiza makontena manne kutoka China
mwezi Novemba -- mawili yaliingizwa kupitia bandari ya Mombasa na mawili kupitia
Dar es Salaam. Makontena yaliyopitia Mombasa yaliondolewa ndani ya siku tisa,
wakati yale yaliyopitia Dar es Salaam yaliendelea kukwama katika bandari ya Dar
es Salaam hadi tarehe 7 Januari.
"Lengo langu lilikuwa ni kuuza bidhaa katika
wiki la kati ya Krismasi na mwaka mpya lakini sasa kama nikipata bidhaa hizo
zote nitazifanyia nini?" aliiambia Sabahi. "Bandari [ya Dar es Salaam] imeua
kabisa biashara yangu."
Nyerere alisema kama bandari ingekuwa na
utaratibu mzuri na kufanya kazi kwa ufanisi, ingeweza kuzalisha hadi shilingi
bilioni 100 (dola milioni 63) kwa mapato ya mwezi.
Haron Ishimwabula, ambaye kampuni yake ya
usafirishaji nje na uingizaji wa bidhaa inahudumia Rwanda, Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Malawi na Zambia, alisema kwamba kwa sababu ya kutofanya
kazi kwa ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam, anatumia bandari ya Mombasa
ili kuingizia bidhaa kwa haraka hata kama inaongeza gharama katika biashara
yake.
Mchumi Benson Mahenya, mkurugenzi wa Andrew's
Consulting Group, alisema serikali inapoteza mapato mengi sana kwa bandari
shindani katika nchi za eneo hili. Kwa kuwa ni eneo la kimkakati, bandari
inaweza kuzalisha hadi asilimia 60 katika bajeti ya taifa, aliiambia Sabahi,
lakini kwa sababu ya kutokuweko kwa ufanisi mapato yanayotarajiwa kupatikana
hayafikiwi.
Mahenya alipongeza jitihada za Mwakyembe
kuboresha utendaji wa bandari na kuwaomba kila mmoja kuunga mkono mabadiliko
yanayokusudia kuondoa ufisadi.
Hata hivyo, alisema mfumo wa uchukuzi katika
bandari pia unahitaji maboresho. Kwa mfano, badala ya kutumia magari makubwa ya
mizigo, mfumo wa reli unapaswa kuhuishwa kwa ajili ya shehena kubwa na
usafirishaji wa haraka wa bidhaa kutoka bandarini, alisema Mahenya.
Mwakyembe alisema maboresho ya utendaji
bandarini ni endelevu na wizara yake itaendelea kukagua njia za kuboresha
ufanisi. Alisema wizara hiyo inazingatia kufanya kazi katika bandari kwa saa 24
ili kuondoa shehena ya kontena ambazo zinatakiwa kutolewa.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment