DAR ES SALAAM, Tanzania
KATIBU wa wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amewataka
Chadema wasitafute mchawi anayewamaliza nje ya chama chao kwa kuwa
ubaguzi ulioota mizizi kwa muda mrefu ndani ya chama hicho ndiyo
unaowamaliza..
Alisema kwa
kukumbatia ubaguzi aliodai kulelewa na waasisi na viongozi wa kitaifa
ndani ya Chadema, sasa iliyobaki waandae mapema, mazishi ya chama hicho
kwa kuwa hakuna jinsi ambavyo kitanusurika kufa kutokana na dhmabi hiyo
mbayo hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliikemea akisema ni mbaya
sawa na kula nyama ya mtu.
Nape aliyasema
hayo leo Januari 20, 2013, jijini Mwanza kwenye mkutano wa hadhara wa
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na baadhi ya mawaziri,
uliohudhuriwa na maelfu ya wanachi wa jiji hilo na vitongoji vyake
kwenye Uwanja wa mpira wa Nyamagana.
Nape alisema
anashangazwa na viongozi wa Chadema kuendelea kunyooshea vidole CCM kuwa
eti inahusika na mtafaruku na umahututi wa chama chao wakati CCM
walishajitahidi kuwataadharisha mapema kuwa ubaguzi wanaoukumbatia,
licha ya kuathiri umoja na mshikamano ni dhambi ambayo itakisambaratisha
chama hicho.
"Hamuwezi kuwa
na chama ambacho ili kiongozi wake adumu na kuheshimika lazima awe
anatoka ukanda fulani au ukoo fulani ndio adumu, vinginevyo anasukiwa
mizengwe na mwisho kutimuliwa" alisema Nape na kuongeza "walianza na
kina Chacha Wangwe na Watanzania wote wanajua leo kilichompata Chacha
Wangwe, sasa wameanza kumwandama Zitto na wanaoitwa vijana wake, na pia
nasikia wamejipanga kumfukuza Shibuda wiki ijayo."
"Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere alishasema dhambi ya ubaguzi ni kubwa, na ni sawa na
kula nyama ya mtu, ambapo mtu akishaila anazoea kiasi kwamba haachi,
basi nao Chadema hawana namna ya kuachana na ubaguzi unaoendelea ndani
ya chama chao, hivyo watasambaratika kwa laana hiyo ya Mwalimu", alisema
Nape.
Nape alilionya
kwamba, ikiwa Chadema wanabaguana kiasi hicho ndani ya alichokiita
kichama kidogo, kama hicho watafanyaje wakipewa dhamana ya kutawala
nchi. " Ikiwa wanabaguana ndani ya kichama kidogo kiasi hichi ambacho
hakijai hata mkononi, watafanyaje wakipewa dhamana ya kuongoza hata
kipande cha nchi yetu?" alihoji.
Nape alidai
kuwa ubaguzi ndani ya Chadema umejikita kwenye ukanda, ukabila na hata
udini na kwamba ubaguzi huo unajionyesha zaidi kwenye safu ya uongozi wa
chama hicho na maeneo mengine. "Sasa leo nimeamua kuwapa ushauri wa
bure kabisa Chadema wasiendelee kutafuta mchawi nje ya chama chao",
alisema.
Mkutano huo
ambao umehusisha wananchi kutoka Wilaya za Ilelema na Nyamagana, ni moja
ya mikutano ya Mangula ambayo amekuwa akiifanya tangu aanze ziara ya
kwanza katika mkoa wa Mwanza ambapo tayari ameshapita katika wilaya za
Magu, Ukerewe na Sengerema.
Post a Comment