Haruna Chanongo aliyeruka kufunga bao la kwanza la Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry wa Bin Zubeiry,
Zanzibar
MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC wameanza vyema
michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kuwachapa mabingwa wa Zanzibar, Jamhuri
ya Pemba mabao 4-2 usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana
mabao 2-2, zikicheza huku zikinyeshewa na mvua iliyoanza kabla hazijaingia
uwanjani.
Jamhuri ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya
17, mfungaji Mfanyeje Mussa Yussuf kwa shuti la umbali wa mita
17.
Simba ilisawazisha bao hilo dakika ya 27, mfungaji
Haruna Athumani Chanongo aliyeunganisha kwa kichwa kona maridadi iliyochongwa na
kiungo Kiggi Makassy kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao hilo, Simba walizidisha mashambulizi
langoni mwa Jamhuri na iliwachukua dakika mbili zaidi kupata bao la kuongoza,
baada ya Chanongo kufumua shuti kali akiwa umbali wa mita 20 upande wa kushoto
mwa Uwanja, ambalo lilimshinda mlinda mlango Jaffar
Said.
Huku ikielekea kama Simba itatoka uwanjani baada ya
ngwe ya kwanza ikiwa inaongoza 2-1, Mfanyeje tena aliwainua vitini wapenzi wa
timu hiyo ya Chasasa, Pemba kwa bao tamu la kusawazisha akimalizia mpira wa
adhabu uliopigwa na Abdallah Athumani, akamtungua kiulaini kipa wa Simba,
William Mweta.
Kipindi cha pili, Simba walirudi kwa kasi ya kusaka bao
la ushindi iliwachukua dakika 12 tu kufanikisha malengo yao, baada ya Nahodha wa
timu hiyo leo, Shomary Kapombe aliyecheza kama kiungo mkabaji badala ya beki wa
kati, kufunga kwa shuti la chini la mpira wa
adhabu.
Adhabu hiyo ilifuatia mshambuliaji wa kimataifa wa
Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la hatari
na beki mmoja wa Jamhuri.
Sunzu aliwainua vitini wapenzi wa Simba dakika ya 66,
baada ya kuuwahi mpira uliokuwa unaelekea kutoka nje na kugeuka nao kuutumbukiza
nyavuni kiufundi.
Kabla ya mchezo huo, Makamu wa kwanza wa rais wa
Zanzibar, Seif Sharrif Hamad alizindua mashindano hayo kwa kupiga penalti na
kumfunga kipa wa Jamhuri, Jaffar. Akiongozwa na raisi wa Chama cha Soka Zanzibar
(ZFA), Aman Ibrahim Makungu, Mh Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF,
alizikagua timu zote mbili kabla ya kuanza
kucheza.
Kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig alikuwa
jukwaani akiishuhudia timu, ikiongozwa na watakaokuwa wasaidizi wake, Mganda
Moses Basena na mzalendo, Jamhuri Kihwelo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba SC kilikuwa;
William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Mussa Mudde/Abdallah Seseme dk81,
Komabil Keita, Shomary Kapombe, Haroun Chanongo, Mwinyi Kazimoto/Jonas Mkude 67,
Felix Sunzu/Ramadhan Singano dk81, Haruna Moshi na Kiggi Makassy/Christopher
Edward dk27.
Jamhuri FC; Jaffar Said/Suleiman Maabad dk 75, Msafiri
Leonard, Hamad Omar, Hussein Omar, Mfaume Shaaban, Soud Amoud, Bakari Hamisi,
Ally Bilal/Mbara Ali dk82, Ally Ahmed ‘Shiboli’, Mfanyeje Mussa na Abdallah
Athumani.
Katika mchezo uliotangulia, Tusker ya Kenya iliichapa
Bandari ya hapa mabao 5-1, mabao ya Jesse Were 29 na 43, Ismail Dunga 35 Michael
Olunga dakika ya 89 na Andrew Tolowa dakika ya 90, wakati la Bandari lilifungwa
na Amour Janja dakika ya 83.
Post a Comment