|
Thomas Murugwa,
Urambo
MKAZI
wa Kitongoji cha Kinondoni, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Zengabuyaga Meli,
ameuawa kwa kukatwa mapanga, wakati akijaribu kumwokoa mjukuu wake, Lugolola
Bunzari (albino) ambaye naye alifariki baada ya wahalifu kumkata mkono na
kuondoka nao.
Kwa mujibu
wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, wahalifu hao walivamia
nyumbani kwa baba wa albino huyo, Bunzari Shinga na kuvunja mlango kisha kumkata
mkono wa kushoto karibu na bega mtoto huyo mwenye ulemavu wa ngozi na kuondoka
nao.
Alisema
kuwa kabla ya kuondoka na kiungo hicho, walimjeruhi kwa mapanga sehemu
mbalimbali za kichwani, sikioni na mguuni hali iliyomfanya kutokwa na damu
nyingi na hivyo kupoteza maisha.
Kamanda
alifafanua kuwa, watu hao pia walimuua kwa kumcharanga mapanga babu wa mtoto
huyo, Zengabuyaga wakati akijaribu kumnusuru mjukuu wake.
Rutta alisema kuwa watu
hao zaidi ya wanane ambao bado hawajafahamika, wakiwa na silaha aina ya gobole
na mapanga walivamia nyumbani kwa Shinga katika Kitongoji cha Kinondoni na
kufanya mauaji hayo.
Aliongeza kuwa katika
mauaji hayo ambayo inadaiwa yametokana na imani za kishirikina, wauaji pia
walimjeruhi sehemu ya nyonga mguu wa kulia kwa risasi baba wa mtoto huyo, Shinga
ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Kamanda alisema kuwa
babu wa mtoto huyo alikatwa sehemu za sikio, mguu wa kulia na mkono wa kulia na
kuachwa ukining’inia katika purukushani za kumsaidia mjukuu wake
asiuawe.
Pia katika tukio hilo
lililotokea saa kumi ya usiku wa kuamkia juzi, wahalifu hao walimjeruhi kwa
mapanga sehemu ya mguu wa kushoto bibi wa mtoto huyo, Dama Zenga ambaye naye
amelazwa hospitali ya Kitete.
Kamanda Rutta alisema
kuwa chanzo cha mauaji hayo ya kusikitisha ni imani za kishirikina, na kwamba
familia hiyo inaishi porini jambo ambalo lilikuwa gumu kwa jirani zao kutoa
msaada kwa urahisi wakati walipopiga kelele.
|
on Saturday, February 2, 2013
Post a Comment