Chadema kimeanza kuandaa mashambulizi ya kuchukua madaraka ya nchi kutoka mikononi mwa CCM, lakini hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa kuwa CCM nayo inaelekeza mashambulizi kwa Chadema kama chama, na wanachama binafsi, hasa Dk Willibrod Slaa ambaye jina lake limeendelea kusimama kama alama ya chama hicho.
Chama hicho kimetokea kuwa ni mwiba mkali kwa CCM, na kuwa kivutio kwa idadi kubwa ya vijana kutokana na ushawishi unaojidhihirisha kutoka kwa wabunge na makamanda wa chama hicho.
Mbali na ushawishi huo, pia chama hicho kimekuwa kikijivunia mipango yake mahususi, kama operesheni za ujenzi wa chama, kurudisha madaraka kwa wanachama kupitia Sera yake ya majimbo na shughuli zingine.
Januari 27 na 28, mwaka huu chama hicho kimefanya vikao vyake vya juu – Kamati Kuu na Baraza Kuu – na kujadili ajenda mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu 2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika hatua iliyopo ni kuzingatia uamuzi ya kuwapata viongozi na kuweka mpango kazi wa kuongeza nguvu ya umma.
“Tunaanza ujenzi wa chama ili kujiimarisha zaidi katika harakati za kushinda uchaguzi mkuu ujao, lakini pia tunajiweka sawa kwa namna tutakavyosimamia ahadi zetu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kuishinikiza Serikali kutekeleza,” anasema Mnyika. Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametangaza vita ya kisiasa, akisisitiza kuwa “Mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.”
Anasema chama hicho kimeweka mikakati ya kujijenga kuanzia matawi hadi taifa na kutawashughulikia wanachama wanaodaiwa kutumiwa na CCM kuanzisha migogoro ndani ya chama.
Kauli hiyo ya mwenyekiti, ni kinaashiria kuwa ndani ya chama hicho kuna migogoro ambayo isipoangaliwa na kutatuliwa katika kipindi hiki, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema inaweza kuwa kikwazo kwa harakati na mipango yake ya kushika dola.
Uamuzi kufuata Katiba
Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema Chadema inapaswa kuhakikisha inafanya uamuzi na kutekeleza mipango yake kwa kufuata Katiba, ili kuhakikisha inaendelea kuimarika zaidi mpaka kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Anasema endapo migogoro inayodaiwa kuwamo itaendelea ndani ya chama hicho, na chenyewe kikafanya uamuzi bila kufuata katiba yake, basi hakutakuwa na mafanikio ndani ya chama hicho.
MWANANCHI
MWANANCHI
Post a Comment