WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema kila Halmashauri hapa nchini ina wajibu wa kuhakikisha kuwa mipango inayowekwa inalenga kusadia watoto walio katika mazingira hatarishi.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Februari mosi, 2013) wakati mamia ya wazazi na wanafunzi walioshiriki uzinduzi wa Mpango Kazi wa Pili wa Taifa wa Watoto walio katika Mazingira Hatarishi uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Mpango
Amesema wadau wakuu katika kutekeleza mpango kazi huo wa miaka mitano (2013 -2017) ambao ni Halmashauri zote nchini, Serikali Kuu, Bunge, Mahakama, washirika wa maendeleo, asasi zisizo za kiserikali na madhehebu ya dini wana mchango mkubwa wa kuhakikisha hali za watoto hao zinabadilika.
“Kila Halmashauri itekeleze wajibu inavyotakiwa. Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Madiwani ni lazima tuhakikishe mipango yetu inalenga kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi,” alisema.
Waziri Mkuu alisema wadau wengine wakuu katika kutekeleza mpango kazi huo ni Serikali Kuu ambapo alizitaka Wizara Mtambuka zinahusika na suala hili zijipange kuhakikisha mpango huo unatekelezwa na kusaidia kubadilisha maisha ya watoto hao.
Alisema Bunge kwa upande wake, ambalo liliwakilishwa kwenye uzinduzi huo na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, litasaidia kuhakikisha fedha inayopangwa inapatikana kwa wakati na inatumika vizuri.
Akisisitiza kuhusu jukumu la kulea na kutunza watoto ni la kila mmoja, Waziri Mkuu alisema: ”Watanzania mmoja mmoja ni lazima tuonyeshe upendo kwa watoto kwa sababu mtoto wa mweinzi ni mtoto wako. Usimuone mtoto wa mwenzio anafanyiwa ukatili au ana hali mbaya ukasema shauri yake, huyu si wa kwangu”.
Alizitaka pia Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zikae pamoja na kuwaita wadau wake ili ziweze kujadiliana njia bora ya kutoa huduma vizuri zaidi kwa jamii wanazozihudumia kwenye mikoa mbalimbali badala ya kuachia asasi nyingi kuwa zimejirundika katika mikoa michache tu.
Mapema wakisoma risala yao, watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu walisema tangu mpango huo uanze mwaka 2007, wamenufaika kwa kupatiwa vifaa vya shule, sare za shule, mablanketi na ada.
Walisema mpango huo umewasaidia kuwafanya wajiamni wawapo shuleni tofauti na hapo awali ambapo wenzao walikuwa wakiwadhihaki na kuwatenga kwa kukosa sare au kuwa wachafu wawapo shuleni kwani hawakuwa na nguo za kubadilisha.
Walitumia fursa hiyo kuomba wanapofaulu, wapatiwe nafasi za bweni ili wawe na uhakika wa kumaliza shule, wasidaiwe michango mbalimbali shuleni na wakipata nafasi ya kwenda elimu ya juu, wapatiwe ufadhili na serikali kwa asilimia 100.
Post a Comment