Imeandikwa na Happiness Katabazi
HATIMAYE upande wa Jjamhuri katika kesi ya
uchochezi na kuiba malighafi zenye thamani ya Sh. milioni 59
inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa
Ponda na wenzake 48, umetangaza rasmi kuifunga kesi yake.
Hayo yalisemwa na Wakili Mwandamizi
wa Serikali, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, muda mfupi baada ya
shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuru D/C F8586 Ismail wa kituo cha Polisi
Chang’ombe kumaliza kutoa ushahidi wake ambapo jana jumla ya mashahidi
watatu kwa mpigo walitoa ushahidi wao.
Wakili Kweka alieleza kuwa hadi
kufikia jana upande wa Jamhuri ulikuwa umeleta mashahidi 17 na
vielelezo 13 ambavyo vilipokelewa mahakamani kama vielelezo
vimetosheleza upande wa Jamhuri kufikia uamuzi huo wa kuifunga kesi yao.
Baada ya wakili Kweka kutoa maelezo
hayo wakili wa Ponda, Juma Nassor aliiomba mahakama iwapatie muda hadi
Machi 4 ili waweze kwenda kujiandaa na kufanya utafiti utakaowawezesha
kuwasilisha maombi ya kuwaona wateja wao wote 49 hawana kesi ya kujibu.
Hata hivyo, Hakimu Nongwa alisema
jukumu la kupanga tarehe ya kuja kufanya majumuisho ya mawakili wa pande
hizo mbili katika kesi hiyo ya kuwaona washitakiwa wanakesi ya kujibu
au la ni vyema ikaachiwa mahakama. Hakimu huyo akatoa amri kuwa
majumuisho hayo yatafanyika Februali 27, 2013, saa mbili asubuhi na
kuutaka upande wa utetezi kuwa wa kwanza kuwasilisha majumuisho yao kwa
njia ya mdomo.
Kabla ya Hakimu Nongwa kukubali ombi
la upande wa Jamhuri majira ya saa nane mchana, la kuifunga kesi yake,
alisikiliza ushahidi wa mashahidi watatu wa waliokuwa wameletwa na
upande wa Jamhuri ambao ni shahidi wa 15 ambaye ni F3929 D/C Constebo
Eliaeli (35), shahidi wa 16 ambaye ni Stationi Sajenti Amos wa kituo
cha Polisi Kati na Shahidi wa 17 ambaye ni askari mpelelezi Na. F8586
D/C Ismail.
Kwa upande wake shahidi wa 17, D/C
Ismail aeleza mahakama kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa kazi na Mkuu
wake wa kazi na saa 2-9 alasiri alikuwa katika kituo cha Polisi
Kijinyoma alipewa jukumu la kuwahoji washitakiwa ambao walikamatwa
katika kiwanja cha Chang’ombe Marskas wakikabiliwa na makosa ya kuingia
kwa jinai katika kiwanja hicho .
Ismail alidai kuwa yeye alimhoji
mshitakiwa aitwaye Fiswaa ambaye alimweleza kuwa kati ya tarehe, mwezi
na saa isiyofahamika akiwa nyumbani kwake Mlandazi Mkoani Pwani, akiwa
anasikiliza Redio Iman, alisikia tangazo lilokuwa likiwataka waumini wa
dini ya Kiislamu kwenda kuongeza nguvu ya kujenga msikiti katika kiwanja
cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya waislamu na si BAKWATA, lakini
kilikuwa kimevamiwa.
Shahidi huyo alidai kuwa, mshitakiwa
huyo alimweleza kuwa aliitikia wito huo na kufunga safari toka nyumbani
kwake Mlandizi na kwenda hadi kwenye kiwanja hicho kilichopo Dar es
Salaam, na kuungana na wenzake ambapo kiongozi wao aliyekuwa akiwaongoza
walipokuwa kwenye kiwanja hicho ni mshitakiwa wa kwanza ambaye ni
Sheikh Ponda.
“Sululu, mapanga vilitumika kama
vifaa vya kujengea msikiti wa muda katika kiwanja hicho na ndipo usiku
wa kuamkia Oktoba 17 mwaka jana, tukiwa tumekaa kwenye kiwanja hicho
nikasikia sauti ikisema kuwa panda kwenye gari, panda kwenye gari na
sikuwa na kumbukumbuku yoyote...,’ alidai Ismail kuelezwa na Fiswaa.
Maelezo ya mshitakiwa huyo yalipokelewa kama kilelezo cha 13 na
hakikupingwa na mawakili wa utetezi.
Kwa upande wake shahidi wake Shahidi
wa 16, Station Sajenti Amos, alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana alipewa
jukumu la kumhoji mshitakiwa Hussein Ally ambaye mshitakiwa huyo
alimweleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa Masheikh wake wa Msikiti
wa Kinyerezi yakimtaka afike katika kiwanja cha Markas na alienda
akakutana na wenzake ambapo walianza kufanya usafi ili waweze kujenga
msikiti na walikuwa wakiongozwa na Sheikh Ponda kufanya ujenzi na usafi
katika kiwanja hicho ambacho tayari mashahidi wengine kutoka BAKWATA
walishasema kiwanja hicho ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd, na siyo
BAKWATA tena. Maelezo ya mshitakiwa hayo yalipokelewa kama kielelezo cha
12.
Aidha, shahidi wa 15 , D/C Constebo
Elieli alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa jukumu na mkubwa wake
wa kazi la kuandika maelezo ya mshitakiwa Mohamed Ramadhan ambaye
alimweleza kuwa siku hiyo yeye alikwenda kusali katika eneo la kiwanja
hicho akitoa Oysterbay Dar es Salaam. Elieli alieleza kuwa mshitakiwa
huyo alimweleza kuwa alifikia uamuzi wa kwenda kusali swala ya alfajiri
hapo Chang’ombe Markas kwa sababu alikuwa anauguliwa na ndugu yake
anayeishi Keko. Yeye mshitakiwa hakutaka kwenda kuswali Msikiti ya Keko
kwa sababu hali ya usalama ilikuwa mbaya na hivyo akaamua kwenda kusali
katika eneo hilo la Markas.
“Mshitakiwa huyo akanieleza eti baada
ya kusali hapo alfajiri ya Oktoba 17 mwaka jana, ndiyo ghafla
alishitukia anakamatwa na mapolisi. Nilipomhoji kama analifahamu
vuguvugu la Waislamu kudai haki zao, mshitakiwa huyo alikubali
kulifahamu vuguvugu hilo na kwamba yeye pale kwenye lile eneo
alipokamatiwa alikuwa katika kutetea na kudai haki yao ya kurejeshewa
kiwanja kile ambacho ni mali ya Waislamu na si BAKWATA,” alidai Elieli.
Hata hivyo, mahakama ilikataa kuyapokea maelezo hayo kama kielelezo kwa
sababu yana dosari nyingi za kisheria.
Awali Oktoba 18 mwaka jana, ilidaiwa
kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na wakili Kweka mbele ya Hakimu
Nongwa kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano likiwemo kosa
la kula njama,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh. milioni 59 na
uchochezi ambalo linamkabili Ponda na mshitakiwa wa tano, Sheikh Mkadam
Swalehe ambao wanaendelea kuzuiliwa gerezani kwa sababu Mkurugenzi wa
Mashitaka, DPP, Dk Eliezer Feleshi bado hawajaondolea hati ya kuwafungia
dhamana.
wavuti
Post a Comment