WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wame muua kinyama mke wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki M. Meera Sanjeev Kumar kwa kumfunga plasta mdomoni wakiwa katika harakati za kufanya uhalifu nyumbani kwa ofisa huyo.
Taarifa za mauaji hayo zilitolewa polisi na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa alifika Kituo Kikuu cha Polisi Oysterbay kutoa taarifa za mauaji hayo.
Akizungumza jana Kama nda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambayo aliyaita ni ya kinyama na kueleza kuwa maja mbazi hao watashughulikiwa ipasavyo.
“Ni kweli kuna mauaji hayo yametokea eneo la Masaki ambako mama mmoja Meera Sanjeev Kumar (52) ameuawa majira ya saa tano usiku juzi akiwa nyumbani kwake,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema watu hao wanaodhaniwa ni majambazi walifika katika nyumba hiyo iliyoko kiwanja namba 1500 na ku mfunga kamba mikononi na miguuni na halafu plasta mdomoni na puani na kusababisha kifo chake.
“Wakati wa tukio, mume wake aitwaye Sanjeev Kumar(56) hakuwepo nyumbani na aliporudi alimkuta mkewe akiwa kwenye kochi na tayari amekwishafariki,” alisema Kamanda Kenyela na kuongeza;
“Baada ya kukuta hali hiyo, alipatwa na mshtuko na kupiga simu polisi ambao walifika katika nyumba hiyo na kukuta mauaji hayo.”
Alisema baada ya polisi kufika walielezwa kuwa nyumba hiyo ina walinzi watatu, lakini walikutwa wawili wakiwa wamelala huku mmoja wao akiwa hayupo eneo hilo.
“Tulifuatilia na kubaini kuwa wale walinzi walikuwa wako hoi baada ya kula chakula kilichokuwa kimewekwa dawa ya kulevya ambayo yalisababisha walewe na kushindwa kujitambua,” alisema Kamanda Kenyela na kuongeza;
“Mlinzi mwenzao wa tatu ambaye inadaiwa ndiye aliyewapelekea chakula hicho na kuhusika na njama za kufanyika kwa uhalifu huo alitokomea na majambazi hayo na hajulikani aliko hadi sasa.”
Kamanda Kenyela alisema hadi sasa haijulikani kama kuna kitu kilichoibwa kwa kuwa mume wa marehemu huyo bado hajatulia kuweza kueleza kama kuna fedha au kitu chochote kilichoibwa.
Alisema walinzi waliokuwa wanalinda nyumba hiyo wote ni wa Kampuni ya Securex na kitendo kilichofanywa na mmoja wao ni kusaliti lindo lao na kujihusisha na ujambazi jambo ambalo ni hatari.
“Tunamsaka mlinzi huyo kwani amesababisha mauaji na kwamba tabia ya walinzi kujihusisha na uhalifu inatisha kwa kuwa kama wenyewe wanajihusisha na ujambazi basi ni hatari,” alionya Kenyela.
Alisema ni muhimu kampuni za ulinzi zikawa makini na watu zinaowaajiri kwa kuweka takwimu zao vizuri ili wanapofanya uhalifu kama huo wajulikane mapema.
Kamanda Kenyela alisema hivi sasa Kinondoni kuna tishio la baadhi ya walinzi kujihusisha na ujambazi kitu ambacho kinafanya kazi ya polisi kuwa ngumu.
Alisema tishio jingine ni la madereva wa bodaboda ambao nao wamekuwa wakijihusisha kwenye ujambazi.
MWANANCHI
Post a Comment