NIGERIA ilifunga magoli matatu ndani ya dakika 20 katika kipindi cha kwanza wakati walipoisambaratisha Mali 4-1 na kutinga fainali ya Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2000 leo.
Baada ya Mali kuanza mechi vyema na kutishia kupata goli la kuongoza la mapema, Nigeria walizinduka kupitia magoli ya Elderson Echiejile katika dakika ya 25, Brown Ideye (dk. 30) na goli la kujifunga la kutoka kwa beki wa Mali, Momo Sissoko kabla ya mapumziko.
Winga aliyeingia kutokea benchi, Ahmed Musa, ambaye alichukua nafasi ya Victor Moses katika dakika ya 53 aliongeza goli la nne dakika tatu baadaye wakati alipotegua mtego wa kuotea na kufunga kwa kumpiga 'tobo' kipa Mamadou Samassa.
Mali, ambao wanakumbukwa kwa kuzinduka kutoka 4-0 nyuma na kulazimisha sare ya 4-4 dhidi ya Angola katika fainali za mwaka 2010, hawakuonekana kama wangeweza kurejea mafanikio hayo lakini walifunga goli la kufutia machozi kupitia kwa Cheick Diarra katika dakika ya 75.
Nigeria watacheza na mshindi dhidi ya Ghana na Burkina Faso ambazo zilicheza baadaye leo..
Post a Comment