TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa kuamkia leo, Jumatatu, Februari 4, 2013, alikutana kwa muda mfupi na kundi la wasaniii wa muziki la Diamond Group wakiongozwa na kiongozi wa bendi hiyo Nasib Abdu maarufu kwa jina la Diamond.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ikulu Ndogo ya mjini Kigoma, wasanii hao walimshukuru Rais Kikwete kwa msimamo wake usioyumba wa kuunga mkono wasanii wa Tanzania na kuhakikisha kuwa wanafaidika na kazi zao.
Rais Kikwete alikuwa mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambako jana, Jumapili, Februari 3, 2013, alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma na ambako Diamond na kundi lake walitumbuiza.
Mwanamuziki huyo alimshukuru Rais Kikwete kwa juhudi zake nyingi na za wakati wote kuunga mkono wasanii wa Tanzania na hasa kuunga mkono mapambano ya jitihada za wasanii hao kunufaika na kazi zao.
Shukurani kubwa za Diamond zilihusu hatua ya Rais Kikwete kumlipa mtaalamu wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam aliyefanya utafiti wa namna ya kuwasaidia wasanii, hatua iliyopelekea Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) kuanzisha mfumo wa kusaidia kuthibiti kazi za wasanii mwaka huu. Mtaalamu huyo alilipwa Sh. milioni 20 kwa kazi hiyo.
Diamond amemwomba Rais Kikwete kuangalia jinsi gani Serikali inavyoweza kuwasaidia wasanii kupata malipo ya haki kutokana na nyimbo zao zinazotumika kama milio ya simu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
4 Februari, 2013
Post a Comment