Msemaji wa klabu ya simba
Ezekiel Kamwaga akizungumza na Waandishi wa Habari leo
mchana
KIKAO cha Kamati ya
Utendaji ya Simba SC jana, kimefikia uamuzi wa kuitisha Mkutano Mkuu wa dharula
wa klabu hiyo, ambao ajenda yake itakuwa moja tu, kujadili mwenendo wa timu
katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari mchana wa leo, makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam,
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba siku na mahali ambako
Mkutano huo utafanyika vitatajwa wakati wowote kuanzia
sasa.
Aidha, Kamwaga alisema
kwamba hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Simba SC aliyejiuzulu na kwamba
uongozi upo pamoja. “Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa klabu ya Simba
aliyejiuzulu. Uongozi upo pamoja na mambo yote yatajadiliwa kwenye mkutano huo
wa dharula,”alisema.
Akiuzungumzia mchezo wa
marudiano, Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kamwaga alisema kwamba
timu itaondoka Alfajiri ya Ijumaa kwenda Angola kuwavaa wenyeji wao, Recreativo
de Libolo.
Alisema mechi hiyo
itafanyika Jumapili mjini Calulo, umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu wa
Angola, Luanda.
“Kwa mujibu wa kanuni za
CAF (Shirikisho la Soka Afrika) kama umbali wa mji ambao inachezwa mechi unakuwa
ni zaidi ya kilomita 200, timu mwenyeji inatakiwa kumsafirisha mgeni kwa ndege,
kwa hivyo ni matumaini yetu, wenyeji wetu watakuwa tayari wametutayarishia
ndege, kwa kuwa hatuwezi kusafiri kwa basi kwa zaidi ya saa nne,”alisema
Kamwaga.
Kamwaga alisema kwamba,
Mkuu wa msafara wa timu atakuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe, wakati upande wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) utawakilishwa na Mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji pia,
Muhsin Balhabou.
Kamwaga alisema kikosi
kamili cha Simba kitakachokwenda Angola kitatajwa Alhamisi kwa kuwa leo ni
mapema sana, kwani wanahofia anaweza kuumia mchezaji yeyote wakati
amekwishatajwa kuwemo kwenye safari.
Simba SC ilifungwa bao 1-0
katika mchezo wa kwanza na Libolo wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na ili isonge mbele, inatakiwa kushinda 2-0.
Mwaka 1978, Simba iliwahi
kufanya maajabu ikitoka kufungwa 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia mjini Dar
es Salaam katika michuano hiyo hiyo na kwenda kushinda 5-0 ugenini, hivyo
kusonga mbele.
Post a Comment