SABA WAPITISHWA KUWANIA
UONGOZI TASMA
WATAALAMU saba wamepitishwa
kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa
Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) utakaofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar
es Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA, Dk. Paul Marealle, wagombea hao wamepitishwa
baada ya kufaulu katika usaili uliofanyika jana (Februari 5 mwaka
huu).
Mwenyekiti aliyemaliza
muda wake Biyondho Ngome anatetea nafasi hiyo dhidi ya alikuwa Katibu Mkuu wa
chama hicho, Mwanandi Mwankemwa. Nafasi ya Katibu Mkuu ina mgombea mmoja ambaye
ni Nassoro Matuzya wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata
mgombea.
Sheky Mngazija ni mgombea
pekee wa nafasi ya Katibu Msaidizi kama ilivyo kwa Juma Mzimbiri aliyepitishwa
kuwania nafasi ya Mhazini. Naye Hemed Mziray ni mgombea pekee wa nafasi ya
ujumbe wa Kamati Kuu ya TASMA.
Nafasi ya Mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemvutia Joakim
Mshanga pekee.
Wapiga kura ni wajumbe
sita wa Kamati ya Utendaji na wawakilishi watatu watatu kutoka mikoa ya Geita,
Ilala, Iringa, Kagera, Kinondoni, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Temeke. Hivyo jumla
ya wapiga kura wote ni 33.
UCHAGUZI TAFCA SASA KUFANYIKA MACHI 16
Baada ya kukwama mara
mbili, wanachama wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu (TAFCA) wamepewa fursa
ya kufanya uchaguzi wa chama hicho Machi 16 mwaka huu mjini
Dodoma.
Kwa mujibu wa tangazo la
uchaguzi huo, fomu kwa ajili ya waombaji uongozi katika TAFCA zitaaza kutolewa
kesho (Febaruari 7 mwaka huu) na mwisho wa kurudisha ni Februari 11 mwaka huu.
Majina ya waombaji uongozi watakaokuwa wamepitishwa yatatangazwa Februari 12
mwaka huu.
Kipindi cha kuweka
pingamizi ni kuanzia Februari 13 hadi 17 mwaka huu. Usaili kwa waombaji
utafanyika Februari 19 mwaka huu wakati matokeo ya usaili yatatangazwa Februari
20 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF
itasikiliza rufani kama zitakuwepo kati ya Februari 20 na 22 mwaka huu, na
uamuzi wa rufani hizo utatangazwa kati ya Februari 23 na 27 mwaka
huu.
Ada za fomu kwa waombaji
uongozi zitakuwa sh. 200,000 kwa nafasi zote isipokuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Nafasi zitakazowaniwa ni Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini, Mhazini Msaidizi,
Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF na wajumbe wa Kamati ya
Utendaji.
Fomu kwa waombaji uongozi
zinapatikana kwenye ofisi za TAFCA zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam.
Post a Comment