Sekretarieti ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua
uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho
ya Katiba ya TFF toleo la 2012.
Baada ya kupokea barua hiyo
jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF,
Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya
Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya
Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam.
KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA
KUCHOJOA BUKTA
Kocha Mkuu wa Azam, Stewart
John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha
bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu
Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi
mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu
ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea
lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka
jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha
Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa
kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi
wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera
Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa
kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika
mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye
benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro
United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea
lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4
mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina Faso,
Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi
kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph
Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na
kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile timu ya Azam
imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati
yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam
Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia Coastal Union imetozwa
faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi
msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka
jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon
imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha
kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union
iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso ya
Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya
ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka
jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh.
200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi
yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers imepigwa
faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa
za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini
Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini
ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga
waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa
barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano
wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT
Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi
Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa
JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza
kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada
ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na
washabiki.
Kwa vile masuala ya wachezaji
hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na
Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa
hatua.
MWAMUZI FIFA, MAHAGI
WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi Msaidizi wa FIFA,
Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za
chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo
kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na
FDL.
Waamuzi wengine walioondolewa
kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba),
Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa
Sugar).
Walioondolewa kwa kupata
alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto
Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union),
Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs
Mtibwa Sugar).
Masoud Mkelemi aliyekuwa
mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad
ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match
meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.
MAKAMISHNA VPL/FDL
WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi ya makamishna wa VPL
na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo
kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF
baada ya mechi.
Kamishna Mohamed Jumbe
aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya
makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
Makamishna wa mechi kati ya
JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba),
Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro
(Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao
TFF.
Kwa upande wa FDL makamishna
waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya
Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara
vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.
Wengine ni Mwadui vs JKT
Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora
vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino
Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.
Kamati ya Ligi imewakumbusha
makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na
kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya
kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi
(original) TFF.
MECHI YA SIMBA, MTIBWA
YAINGIZA MIL 62/-
Mechi namba 121 ya Ligi Kuu
ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa Sugar kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
Simba imeingiza sh. 239,686,000.
Watazamaji 10,669 walikata
tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh.
15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92.
Kiingilio cha sh. 5,000
ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 9,491
na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio
cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 105 na kuingiza sh.
2,100,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo
ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za
mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya
Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es
Salaam (DRFA) sh. 1,729,504.53.
VUMBI LA VPL KUENDELEA
JUMATANO
Michuano ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 27
mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika viwanja tofauti.
Vinara wa ligi hiyo Yanga
wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio
vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa),
sh. 15,000 (VIP C na B) na sh. 20,000 (VIP A).
Mechi nyingine za ligi hiyo
ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Polisi Morogoro vs Mgambo
Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Toto Africans (Azam Complex, Dar es
Salaam) na Mtibwa Sugar vs Tanzania Prisons (Manungu, Morogoro).
Boniface Wambura
Mgoyo
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)
Post a Comment