Ujenzi wa uwanja wa Ndege wa kisasa wa Mafia, mkoa wa Pwani ukiendelea chini ya usimamizi wa kampuni ya KUANTA ya Uturuki.
-Mkuu wa wilaya aifagilia kampuni ya ujenzi
-Awataka wananchi kukaa mkao wa kunufaika
Na Mwandishi Wetu, Mafia.
Mfuko wa Maendeldeo ya Millenia Tanzania (MCA-T) unaodhaminiwa na Serikali ya Marekani, unatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa wa Mafia, mkoani Pwani hivi karibuni.
Uwanja huo unaojengwa kwa gharama ya kiasi cha dola za kimarekani Milioni 10.4, chini ya usimamizi wa kampuni ya KUANTA Contraction Limited ya nchini Uturuki.
Mtendaji Mkuu wa MCA-Tanzania Bernard Mchomvu, ameyasema hayo alipokuwa akifanya ziara ya kuangalia kasi ya ujenzi wa uwanja huo.
Mtendaji Mkuu wa MCA-Tanzania pia amewataka wahandisi hao kuongeza kasi na ikiwezekana kufanya kazi hiyo usiku na mchana kwa ajili ya kukabili hali ya hewa ya mvua ambayo kwa sasa inatishia amani.
Amesema kwamba MCA-Tanzania imelazimika kufanya ziara za mara kwa mara kufuatilia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo mbalimbali, ili kuwa na majibu ya uhakika kwa mkuu wa mfuko wa MCC.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa Mradi huo Geofrey Asulumenye, amesema kwamba wanatarajiwa kukamilisha ujenzi huo wakati wowote kati ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu.
Mhadisi Asulumenye amesema kazi inayofanyika kwa sasa ni kuweka lami kwenye eneo la kurukia ndege, pamoja na kusawazisha maeneo yanayozunguka kiwanja hicho.
Hata hivyo, Mhandisi Asulumenye amesema hali ya hewa ya mvua na umbali kwa ajili ya kupata mahitaji ya shughuli hiyo ya ujenzi, ni moja kati ya changamoto zilizokwamisha kasi ya kukamilika kwake.
Ameongeza kusema kwamba awali, makubaliano yalikuwa ni kukamilisha kazi hiyo mwezio Disemba mwaka jana, lakini umbali wa upatikanaji wa kokoto, sementi, pamoja na uwezo wa bandari kuhudumia mradi huo zilikwaza kasi ya wakandarasi.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni suala la utaratibu wa mizigo kuingizwa katika mpango maalum na wenye haraka kusafirishwa kutoka Dar es Salaam mpaka Mafia, lakini pia vifaa vya kupakulia mzigo mara kadhaa kuwa katika hali duni.
Mkuu wa wilaya ya Mafia Sauda Mtondoo alimhakikishia Mtendaji Mkuu wa MCA-Tanzania kuwa serikali ya wilaya hiyo kwa ujumla wake kamwe haitasinzia kufuatilia hali ya maendeleo ya mradi huo.
Mtondoo alisema kwamba kila wakati yeye na watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kazi zinazofanywa na wakandarasi hao, lakini pia kuwapatia moyo ili kuwaongezea ari.
Meneja wa Mradi kutoka wakala wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Mhandisi Mbila Mdemu, alisema kuwa kazi kubwa ya maboresho ya uwanja huo tayari imefanyika.
Mhandisi Mdemu alisema, wahandisi wamefanikiwa kuboresha njia ya kurukia ndege kwa kufanya upanuzi, ambapo sasa ndege kadhaa za daraja la kati zinaweza kutua Mafia.
Mambo kadhaa ya msingi ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia wananchi wenye makazi yaliyokuwa jirani na uwanja huo, imefanyika, hivyo ujenzi wa uwanja sasa unaendelea kwa kasi,” alisema Mhandisi Mdemu.