Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, leo ameiwezesha timu yake kutimiza jumla ya Pointi 42, baada ya kuifungia bao pekee dhidi ya Kagera Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliomalizika hivi punde kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi, wakiwania mpira.
Kipa wa Kagera, akiokoa moja ya hatari langoni kwake, mpira uliopigwa na Didier Kavumbagu.
Simon Msuva, akiruka kukwepa kwanja la beki wa Kagera Sugar, Malegesi Mwangwa, wakati wa mchezo huo.
Said Bahanuzi, akijaribu kumpokonya mpira kipa wa Kagera Sugar, Hannington Kalyesubula, aliyekuwa akiokoa mpira huo (kulia) ni Didier Kavumbagu, akijiandaa kumalizia.
Frank Domayo (kulia) akijiandaa kupiga krosi mbele ya Daud Jumanne, wakati wa mchezo huo, ambao umemalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Haruna Niyonzima, katika dakika ya 65.
**********
Niyonzima aliipatia timu yake bao hilo katika dakika ya 65, baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Oscar Joshua, ambapo alimpunguza kiungo wa Kagera, George Kavila na kuachia shuti kali lililotinga katika engo ya nyuzi 90 na kumshinda kipa Hannington Kalyesubula, aliyebaki akiutazama tu mpira huo wakati ukitinga wavuni.
Katika mchezo huo mwamuzi Simon Mberwa, kwa upande wa Kagera alitoa kadi za njano kwa kipa, Hannington Kalyesubula, baada ya kumchezea vibaya Didier Kavumbagu kwa kumdaka mguu, Julius Mlope aliyepata kadi hiyo baada ya kumchezea vibaya Athuman Idd 'Chuji', Shija Mkina, huku kwa upande wa Yanga, aliwalima kadi Beki Nadir 'Canavaro' Athuman Chuji, Haruna Niyonzima, pamoja na David Luhende na Nizar Khalfan waliokuwa katika benchi.
Kagera walifanya mabadiliko kwa kumtoa Julius Mlope na kuingia Paul Ngwai, Darington Enyina na kuingia Themy Felix, na kwa upande wa Yanga, walifanya mabadiliko kwa kumtoa, Said Bahanuzi na kuingia Jerry Tegete, na Didier Kavumbagu nafasi yake ikachukuliwa na Hamis Kiiza.
Pia leo kulikuwa na michezo mingine ya Ligi Kuu, ambapo Mtibwa Sugar walikuwa wakimenyana na Tanzania Prisons, katika uwanja wa Manungu mjini Morogoro, Coast Union, wao walikuwa wakipepetana na Ruvu Shootin, katika Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, na Polisi Moro wao walikuwa wenyeji wa Mgambo Shooting, katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Kwa bahati mbaya hadi Mtandao huu unakwenda hewani kuweka matokeo haya mechi hizo zilikuwa bado hazijamalizika.
credits: SufianiMuhidini
Post a Comment