Serikali imekubali mchakato wa uchaguzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uendelee kwa sharti la kuhakikisha
haki inatendeka kwa wagombea waliofika mbele ya Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana,
Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kati ya
uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri Dk.
Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa
(BMT).
Amesema baada ya maafikiano hayo, TFF
italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo ndilo
lililosimamisha mchakato huo ili litume ujumbe wake kwa ajili ya kusikiliza
malalamiko ya wagombea walioenguliwa.
Rais Tenga ambaye ameishukuru Serikali kwa
kuruhusu mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika
kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali, na kuwa haki si tu
itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza uchaguzi ufanyike kabla
ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. FIFA wakija hata kesho wakituambia
endeleeni sisi tuko tayari. Hesabu zetu ziko tayari, makabrasha yote yako tayari
yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa muda tu kwa wajumbe walioko mbali
waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita ghafla,”
amesema.
Amesisitiza kuwa TFF ilishapanga tarehe ya
uchaguzi, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya walioenguliwa
kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi kwa sababu wanataka
kuendelea kubaki madarakani haya maana hata kidogo.
Hivyo amewataka wagombea wote waliofika kwenye
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa vizuri, kwani FIFA
watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina heshimu Serikali na
itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu FIFA sababu iko kwenye
mpira wa miguu, na FIFA ndiyo wasimamizi wa mchezo huo duniani.
Amewakumbusha wanachama wa TFF, hasa wajumbe wa
Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina katiba, lakini ni lazima pia wafahamu kwanini
kuna FIFA.
Rais Tenga amewahadharisha watu wanaopitapita
mikoani kuomba saini za wajumbe ili kuita Mkutano Mkuu wa dharura wakati wanajua
mkutano ulishaitishwa, lakini ukasimamishwa na FIFA. Jambo hilo kikatiba ni
kosa.
Post a Comment