Waziri wa Ujenzi Dkt. John
Magufuli.
Wizara ya Ujenzi na Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA) imewafukuza kazi na kusitisha mikataba ya Wafanyakazi
Waandamizi saba wa Wizara na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa tuhuma za
ubadhilifu na utendaji kazi mbovu. Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Wizara ya
Ujenzi ya kusafisha Wakala zake na kuongeza ufanisi.
Katika nyakati tofauti
Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi amekuwa akipokea tuhuma za vitendo vya ubadhilifu
miongoni mwa watendaji waandamizi katika Wakala zinazotoa huduma chini ya wizara
hii. Kufuatia tuhuma hizo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
alifanya ukaguzi maalum katika ofisi za TBA Mkoa wa Dar es salaam na Katibu
Mkuu wa wizara Balozi Herbert E. Mrango na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Elius
Mwakalinga waliunda Kamati za kupitia taarifa za CAG na taarifa nyingine.
Kamati hizo zimeweza kubaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za fedha,
manunuzi na uendeshaji.
Maafisa waliofukuzwa kazi
ni pamoja na Bw. Charles Gabriel Lyatuu ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa
Dar es Salaam; Bw. Ladislaus I. Kapongo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa
Dar es Salaam) na Bi. Agness F. Chambo aliyekuwa Mhasibu Msaidizi (TBA mkoa wa
Dar es Salaam). Aidha, kwa Mkurugenzi wa Biashara na Fedha Bibi Yona Orida na
Injinia Charles Makungu ambaye alikuwa ni Mkurugenzi wa Miliki wameondolewa
katika nafasi za uongozi walizokuwa nazo TBA.
Hatua zaidi
zilizochukukuliwa ni kuwashusha vyeo Meneja wa Mkoa wa Pwani Bibi Esteria M.
Nyamhanga na Bw. Samwel C. Samike ambaye alikuwa ni Meneja wa TBA mkoa wa
Mbeya.
Hatua hizi zimechukuliwa
kunatokana na watendaji hao kuhusishwa na tuhuma za ubadhidilifu ambazo
zimebainika kufanyika katika taasisi hiyo. Maeneo ambayo yamebainika kuwa na
ukiukwaji mkubwa ni pamoja na kufanya malipo kwa kutumia mikataba isiyosainiwa
na pande zote, kufanyika malipo kinyume na taratibu za manunuzi na hata malipo
kufanyika kwa fedha taslim kinyume na taratibu.
Aidha, eneo la manunuzi ya
viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya TBA pia yameonyesha kuwa na vitendo
vya ubadhilifu na ukiukwaji wa taratibu. Vipo viwanja vilivyobainika kununuliwa
nje ya taratibu, baadhi ya nyaraka kuonyesha ukubwa tofauti na ule uliolipiwa,
kununua maeneo yasiyofaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Serikali, kuongeza bei
na kufanyika kwa malipo kabla ya mikataba kusainiwa.
Hatua zilizochukuliwa ni
muendelezo wa juhudi za Wizara za kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayoashiria
kuwa na utendaji ulio nje ya maadili yanafuatiliwa na kuchukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha, ili kuboresha
ufanisi katika Wakala hivi karibuni waliteuliwa Mameneja wapya 15 wa TEMESA
katika mikoa mbali mbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwahamisha vituo
mameneja wengine. Kwa upande mwingine, ajira za Watendaji katika vituo vyote vya
mizani tayari zimetangazwa na kwa sasa kazi ya kupitia maombi yaliyowasilishwa
inakamilishwa ili kuhakikisha kuwa watendaji wasio waaminifu hawapati nafasi
katika maeneo hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kwa vitendo vya
ubadhirifu.
Wizara itaendelea kuchukua
hatua za aina hii pale ukiukwaji wa sheria na taratibu za utumishi wa umma
utakapobainika.
Taarifa hii imetolewa
na;
M.S.
Ntemo
MSEMAJI WA WIZARA YA
UJENZI
Post a Comment