Bunge limeingia katika mzozo mwingine na Chadema
baada ya kudaiwa kutoa ripoti polisi likitaka wabunge 28 wa upinzani waitwe ili
wahojiwe katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na fujo
zilizotokea bungeni Februari, mwaka huu. Hata hivyo, chama hicho kikuu cha
upinzani kupitia kwa
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya
Upinzani, Tundu Lissu, kimepinga hatua hiyo kikisema kamati hiyo haipo kisheria
kwa mujibu wa Kanuni ya 113(7) kwa kuwa imemaliza muda wake tangu Februari 8,
mwaka huu na Spika hajaunda nyingine.
Hata hivyo, madai hayo ya Lissu yamepingwa
vikali na Naibu Spika, Job Ndugai ambaye amesema kamati hiyo pamoja na nyingine
mbili za Uongozi na ile ya Kanuni zinatambulika mpaka zitakapoundwa nyingine...
“Hizo tatu ni ‘ongoing’ (zinaendelea) zisipokuwapo, basi Bunge
hakuna.”
Mvutano huo ni wa pili katika siku za
karibuni baada ya ule uliotokea katika Kikao cha Bunge la Februari baada ya
Wabunge wa Chadema kuzua tafrani zilizosababisha kukatishwa kwa kikao kimoja cha
Bunge hilo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Lissu alisema
yeye na wabunge wenzake wapatao 28 watafika mbele ya kamati hiyo lakini
wamekubaliana kuwa hawako tayari kuhojiwa nayo.
Mbali ya Lissu, jana Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara mjini Musoma alisema wabunge wa
chama chake hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo.
Lissu alisema njia iliyotumika kuwaita mbele
ya kamati hiyo kwa kupitia polisi ni kinyume na utaratibu.
“Utaratibu uliotumika ni haramu kwa kuwa
polisi ndiyo wametumika kutujulisha kwamba tunatakiwa tufike mbele ya kamati
hiyo, kutumiwa ujumbe wa polisi si sawa kwani utaratibu wa Bunge unajulikana,”
Lissu alisema na kuongeza:
“Kamati iliposema bungeni kuwa mimi na
wenzangu watatu ni vinara wa fujo ilituhukumu tayari, hivyo kisheria wale
wengine waliobaki walikuwa hawana makosa kwa mujibu wa sheria
zetu.”
Ilidaiwa kwamba Ofisi ya Bunge iliiandikia
Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kutaka kuwaelekeza makamanda wake kufikisha
taarifa hizo.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Advera Senso alisema hakuwa na taarifa hizo na kuahidi
kufuatilia.
Alipoulizwa kuhusu wabunge hao kuitwa kwa
kutumia polisi, Ndugai alisema hakuwa na taarifa hiyo na kuelezea wasiwasi
kwamba suala hilo limefikia hatua hiyo.
“Sidhani kama imefikia huko (kutumia polisi
kuwaita wabunge), kwani kamati ina utaratibu wake wa kumwita mtu yeyote hata
asipokuwa mbunge, kwa kweli sijui na sifikirii kama watakuwa wamefikia
huko,”alisema Ndugai.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kumpigia simu Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari kumpa wito wa kufika mbele ya kamati hiyo ya Bunge na pia
alimwagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karatu (OCD), kuwapa taarifa Mbunge wa
Karatu, Israel Natse na Mbunge wa Viti Maalumu Cecilia
Paresso.
SOURCE::MTANZANIA
Post a Comment