Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi |
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo, mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi, ambaye aliambatana na wakurugenzi wa Sahara Communications (Star TV) na wa Clouds Media, alisema kuwa utaratibu wa sasa unaowalazimisha wananchi wote kupata matangazo ya televisheni kupitia ving'amuzi umekuwa ukiwakosha wengi matangazo hayo na matokeo yake, wao huathirika kwa kukosa pesa za kuendeshea shughuli zao kupitia matangazo ya kibiashara kama ilivyokuwa zamani.
Wamiliki hao wameitaka serikali kutoa uhuru kwa wananchi wote kupata matangazo kwa njia wanazotaka wenyewe za digitali na analojia (antena za kawaida) kulingana na utashi wao na pia uwezo wao kiuchumi badala ya ilivyo sasa ambapo wengi wamekuwa wakikosa uwezo wa kununua ving'amuzi na kuvilipia kila mwezi, hivyo kukosa matangazo yao na mwishowe kuwaingizia hasara wamiliki wa vituo vya televisheni.
Mengi ameongeza kuwa hadi sasa bado wanaendelea kufanya taratibu za kuisihi serikalini itekeleze yale wanayoomba na kwamba, wataendelea kufanya subira kwa miezi kati ya miwili hadi mitatu kuanzia sasa na wakiona kuwa bado serikali iko kimya, watakachokifanya ni kufunga vituo vyao vyote vya televisheni kwani ni bora waendelee na biashara nyingine kuliko ilivyo sasa ambapo kila uchao wamekuwa wakipata hasara.
Serikali ililazimisha kuanza urushaji wa matangazo kupitia ving'amuzi kuanzia Januari Mosi, 2013 na kuzima kwa awamu matangazo yote ya televisheni kupitia njia iliyokuwa ikitumika awali ya analojia isiyohitaji ving'amuzi bali antena za kawaida.
Post a Comment