Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Balozi Seif Idd awataka watendaji wa ZBC kushirikiana na Viongozi wao kuboresha huduma za matangazo ya televisheni.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } alipofanya ziara ya ghafla Kituoni hapo Karume House. (Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Baadhi ya watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) wakisikiliza hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani) alipofanya ziara fupi Kituoni hapo.
Mhandisi wa ZBC Saadat Haji akielezea kero wanazopambana nazo Kituoni hapo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefanya ziara ya ghafla Kituoni hapo.

Mtayarishaji wa Vipindi shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } Nasra Nassor akishauri umuhimu wa kuwa na bajeti maalum katika utengenezaji wa vipindi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na ule wa ZBC wakisikiliza changamoto za watendaji wa ZBC wakati alipofanya ziara fupi kituoni hapo.
Matumaini ya Wananachi katika kupokea na hatimae kuangalia matangazo ya Televisheni kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) yatarejea endapo watendaji wa Shirika hilo kwa kushirikiana na Viongozi wao watajipanga vyema katika kutekeleza majukumu yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla katika Kituo cha Televisheni cha Shirika hilo kilichopo Karume House kuangalia matatizo yaliyopelekea kukosekana kwa matangazo ya Habari Kituoni hapo.
Akizungumza na Uongozi wa Shirika hilo na baadae Watendaji wake, Balozi Seif amesema Serikali iliamua kuunda Shirika hilo lengo likiwa ni kuimarisha zaidi matangazo yake pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utendaji katika sekta ya Habari Duniani.
Balozi Seif amesisitiza kwamba wakati umefika hivi sasa kwa Shirika hilo kuendeshwa kibiashara na hilo litafikiwa iwapo Taasisi zinazoendelea na zile zinazotumia na kuhitaji huduma za matangazo za Shirika hilo zitalipa.
“ Sisi Serikalini tumeshaliagiza Baraza la Wawakilishi ambalo liko chini ya Wizara yangu lianze kulipa fedha wakati linapoendelea na vikao vya Baraza katika matangazo yake ya moja kwa moja. Dodoma Shirika la Utangazaji Tanzania TBC wanalipwa na Bunge wakati wanaporusha matangazo yao utaratibu ambao hata sisi wabunge tunachangia suala hilo “. Amefafanua Balozi Seif.
“ Katika kujenga mahusiano mema baina ya Taasisi hizo inaweza kuruhusiwa kutangazwa bure wakati wa kipindi cha maswali na majibu “. Amesisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewaonya watendaji hao kuwepuka tabia ya fitna baina yao na Viongozi, jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa kazi zao.
Amekemea kwamba Kiongozi yeyote ambae atapenda kutanguliza fitna na majungu mbele aelewe kwamba anajiingiza katika mfumo mbaya wa kazi unaosababisha kuyeyusha haki za wafanyakazi wake.
Hata hivyo Balozi Seif amewapongeza Watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa utendaji wao wa kizalengo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa.
Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alisema Vituo vya Matangazo ya Televisheni haviwezi kufanya kazi zake kwa mpangilio wa bajeti kama zinavyofanya Idara nyengine.
Alisema Uongozi wa Shirika hilo umekuwa ukitoa Taarifa za maandishi wakati yanapotokea matatizo hasa suala kubwa la vifaa na uharibikaji wa mashine lakini ufumbuzi wake huchukuwa muda mrefu kutokana na mfumo wa matumizi uliopo.
Hata hivyo Ndugu Chande alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Shirika hilo tayari umeshachukuwa hatua za dharura kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwasiliana na makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyohitajika kituoni hapo kwa wakati huu wa dharura.
Kwa upande wao watendaji wa shirika hilo la Utangazaji Zanzibar wameelezea changamoto wanazopambana nazo kituoni hapo ambazo zimekuwa zikirejesha nyuma hamu na utendaji wao wa kazi za kila siku.
Walizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu usafiri wa uhakika wa kufuatilia Vipindi, Habari na hata kurejeshwa majumbani wakati wa usiku, ukosefu wa Bajeti za Vipindi, uchakavu wa Mashine za Matangazo, Haki za Wafanyakazi kama posho na fedha za likizo pamoja na majungu na fitina baina ya Viongozi na Wafanyakazi.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top