Na Baraka Mpenja wa fullshangwe Dar es Salaam
Makampuni makubwa yanayojitokeza
kudhamini timu kubwa za ligi kuu soka Tanzania bara yametupiwa lawama
kwa kukimbia majukumu yao ya kuwekeza katika soka la vijana ambalo ndio
msingi wa kupanda kwa kiwango cha mchezo huo nchi yoyote duniani.
Akizungumzia na mtandao huu kutoka
jijini Mbeya, kocha msaidizi wa klabu mpya ya ligi kuu msimu ujao, Mbeya
City na mkurugenzi wa kituo cha kulea na kuibua vipaji cha “Forest
Youth Academy”, mwalimu Maka Mwalwisye amesema makampuni yangekuwa na
nia ya kuendeleza soka yangewekeza katika soka la vijana ili kupata
wachezaji makinda.
“Siku zote nyumba haiwezi kusimama bila
msingi, na huwezi kuvuna mahindi bila kupanda, lazima vijana waandaliwe
kwa juhudi zote, kama makampuni yatajitokeza kusaidia vitua vya soka la
vijana itasaidia zaidi kusonga mbele”. Alisema kocha Mwalwisye.
Kocha huyo alitolea mfano kikosi cha
sasa cha Taifa stars kilichosheheni makinda wengi ambao msingi wao wa
kucheza kandanda umeanzia soka la vijana husasani michuano ya Copa Coca
Cola.
“Watu wanasahau, wakati kocha Kim
Paulsen akikabidhiwa majukumu ya kukinoa kikosi cha Stars alikuwa kocha
wa timu za vijana, alitumia muda mwingi kuwafundisha vijana ambao
baadaye aliamaua kuwatumia timu ya taifa, sasa timu inafanya vizuri,
lakini bado makampuni yanashindwa kujiingiza katika soka la vijana”.
Aliongeza Mwalwisye.
Pia alisisitiza kuwa timu ya taifa
imejaza makinda wanaoonesha soka safi, lakini soka linakwenda na wakati,
hivyo kama jitihada za kuwekeza soka la vijana zitasahaulika, basi
tutarudi wakati ule wa kuzomea Taifa stars kwani itakosa wachezaji
wengine.
Kocha huyo aliongeza kuwa yeye kama
mdau mkubwa wa soka na mwalimu wa mchezo huo aliamua kuanzisha kituo cha
kulea na kuibua vipaji mwaka 2001 na sasa amaepata mafanikio makubwa
sana kufuatia kuzalisha wachezaji wengi wanaocheza ligi kuu na ligi
daraja la kwanza.
“Nimefanikiwa kuwa na kituo changu
ingawa bado ninahitaji msaada mkubwa katika suala la vifaa kama mipira
na chezi. Mimi ni mtaalamu na huwa nashona mwenyewe mipira pale
ninaposhindwa kupata vifaa kwa wakati, hakika kuendesha kituo sio kazi
nyepesi kama watu wanavyofikiria”. Alisema Mwalwisye.
Akipendekeza nini kifanyike, Mwalwisye
amewataka wadau wa michezo na vyombo vya habari kufanya makongamano ya
michezo ili wadau wakutane na kujadili mstakabali wa soka la vijana.
Pia alivitaka vyombo vya habari
kuwaelimisha watu wenye makampuni ili wajiingize kujenga misingi ya soka
la taifa kwa kuwekeza katika soka la vijana ambalo ndio kama msingi wa
nyumba.
Mnamo mwaka jana Kocha Maka Mwilwisye
alikiongoza kikosi cha timu ya vijana ya mkoa wa Mbeya katika michuano
ya Copa Coca Cola iliyofanyika jijini Dar es Salaam, lakini alitolewa
hatua ya awali ya michuano hiyo.
Post a Comment