Shrikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu
(Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo
mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa
ajili ya kusimamia maendeleo.
Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4
mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali
wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na
Wahariri wa Michezo.
Rais Tenga amesema mpango huo
unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada
wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa
umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA.
Amesema mpango wa sasa ni wa
kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani
iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo
imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo mbalimbali vya kusimamia
mchezo huo.
“Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu
tu, lakini tumeongeza mashindano ya aina mbalimbali kama U17, U20, Kombe
la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia
tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo katika mpango wa sasa ni
kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,” amesema.
Rais Tenga amesema TFF imefika
hapa kutokana na watu kujitolea ambapo ametaka moyo huo uendelezwe,
lakini akasisitiza washirika wote kuwa na mpango huo na kuusoma kwani
umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana kazi ya kufanya katika
mpango huo.
“Naomba washirika wote wasome
mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya kusoma, toa maoni yako.
Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na maoni ya watu. Kama una
mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la kujenga, isiwe kazi ya kulaumu
tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko yanafanyika kutokana na mawazo
mapya,” amesema.
Amesema maendeleo ya mpira wa
miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo unahitaji ushiriki wa watu kutokana na
ukweli kuwa uongozi wa mpira wa miguu Tanzania bado ni wa kujitolea.
Rais Tenga amesema ahadi ya TFF
ni kushirikiana na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa
faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi kwa ujumla.
Amewashukuru wote waliotoa maoni
kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na
Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday
Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF, Salum Madadi unapatikana kwenye CD na
nakala laini (soft copy).
Post a Comment