* WABUNGE WAUNGANISHA NGUVU KUTAKA KUMSULUBU BUNGENI
RIPOTI ya tume
iliyoundwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa mwaka 2006 kuchunguza
ujenzi wa maghorofa katika Jiji la Dar es Salaam, imemweka mahala pabaya na
inaweza kumtoa kafara, Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, Tanzania Daima
Jumatano limedokezwa.
Pinda anatolewa kafara
katika sakata la jengo la ghorofa 16 lililoporomoka katikati ya Jiji la Dar es
Salaam wiki iliyopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 40.
Kutokana na janga hilo,
Pinda analalamikiwa kukalia ripoti ya Tume ya Lowassa ambayo ilikuja na
mapendekezo ya kukabiliana na maghorofa yaliyojengwa chini ya
kiwango.
Duru za siasa kutoka
ndani ya Bunge zinasema kuwa tayari kuna baadhi ya wabunge bila kujali itikadi
zao, wameunganisha nguvu kutaka kumsulubu Waziri Pinda katika mkutano ujao wa
Bunge kupitia hoja binafsi au maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri
Mkuu.
Mmoja wa mawaziri
waandamizi wa serikali ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema: “Pinda
anastahili kubeba mzigo, kwani baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo alimwajibisha
nani tangu 2008 hadi sasa?
“Kwa uzembe huu, Pinda
ameshiriki kwa kuwa hakuwawajibisha waliojenga kinyume na utaratibu hadi
Watanzania wengine wakafa. Zamu hii hata akilia anahusika.” Mbunge wa Vunjo
Augustino Mrema (TLP) alimshangaa Waziri Pinda kwa kushindwa kuchukua hatua
zilizopendekezwa na tume ya Lowassa kwani ilipendekeza baadhi ya majengo
yabomolewe na wahusika wachukuliwe hatua.
Alisema athari ya ukimya
huo ni kuendelea kuangamia kwa Watanzania kunakosababishwa na uzembe wa viongozi
wa serikali.
“Hili tatizo la
kushindwa kuchukua uamuzi mgumu litaendelea kutugharimu kila siku, yale
maghorofa yaliyotakiwa kubomolewa kipindi kile hayajaguswa na hayataguswa kwa
sababu ya kubebana, hili hatuwezi kulinyamazia, lazima tukawashe moto bungeni,”
alisema Mrema.
Alisema Watanzania
hawapo tayari kuletewa danganya toto ya tume nyingine ikalete majibu ambayo
tayari yako mezani kwa Pinda.
Mbunge wa CCM aliyeomba
jina lake lihifadhiwe, alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata watendaji
wa Manispaa ya Ilala hakitoshi kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ataendelea kubaki ofisini.
Mrema ambaye amepata
kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa nyakati tofauti,
alisisitiza kuwa Waziri Tibaijuka anapaswa aige mfano wa Rais mstaafu Ali Hassan
Mwinyi na Lowassa walioamua kuachia ngazi kutokana na uzembe wa watendaji
wao.
“Kwa wenzetu leo
inapotokea boti ikazama kwa uzembe na kupoteza maisha ya watu watatu waziri
mwenye dhamana anawajibika, iweje sisi leo tuwachekee mawaziri wetu?” alihoji
mbunge huyo.
Mbunge wa kuteuliwa na
rais, James Mbatia, ameapa kuwasha moto katika Bunge lijalo hadi
kieleweke.
Mbatia ambaye pia ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema lazima Waziri Mkuu atoe majibu ya msingi kwa
Watanzania kwanini hakutekeleza maazimio ya tume ya Lowassa.
Alienda mbali na kuhoji
utendaji wa kitengo cha maafa cha Waziri Mkuu kwani kimekuwa kikishughulika
kutoa vyakula vya misaada kwenye maafa badala ya kudhibiti
yasitokee.
“Tangu tume zianze
kuundwa kuhusu maafa ni akina nani walichukuliwa hatua? Kuanzia tume ya MV
Bukoba hadi tume ya matokeo ya kidato cha nne, Watanzania tumechoka kuneemesha
mifuko ya wajumbe wa tume na kufilisi rasilimali zetu, hivyo Pinda, Tibaijuka
lazima wajiuzulu,” alisema.
Wakati wabunge hao
wakitaka Pinda na Tibaijuka waachie ngazi, habari zaidi ndani ya serikali
zinasema kuwa ripoti ya Tume ya Lowassa haikufanyiwa kazi kwani baadhi ya
majengo yaliyopendekezwa kubomolewa, yanawahusu viongozi wa juu
serikalini.
“Ile ripoti
iliwasilishwa wakati Lowassa bado yuko madarakani. Alishindwa kuifanyia kazi na
haiwezi kufanyiwa kazi kwani baadhi ya majengo yanawahusu viongozi au
yanamilikiwa na watu wa karibu wa viongozi, na ndio wachangiaji wakubwa wa fedha
wakati wa kampeni,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Akifanya majumuisho
katika hotuba ya matumizi ya ofisi yake bungeni kwa mwaka 2008/09, Pinda
alizungumzia jinsi Tume ya Lowassa ilivyofanya kazi katika sakata la ghorofa
kuanguka jijini Dar es Salaam.
Pinda alilithibitishia
Bunge kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yalibainika kuwa
yalijengwa kinyume na taratibu za ujenzi.
Kwa mujibu wa ripoti
iliyoundwa na Lowassa, kati ya maghorofa 505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa
hayana nyaraka za ujenzi.
Lowassa aliunda tume
baada ya jengo la hoteli ya Chang’ombe Village Inn, Keko, Dar es Salaam kuanguka
mwaka 2006 na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa. Ilidaiwa kwamba
ulikuwapo ukiukwaji katika ujenzi wake.
Pinda aliliambia Bunge
kuwa tume hiyo ya Lowassa ilibaini pia maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka masharti
ya ujenzi huku mengine 22 wenyewe hawakupatikana na yalikuwa yamejengwa bila
kuzingatia sheria za ujenzi pamoja na uzembe wa baadhi ya watendaji wakiwamo
wahandisi wa manispaa husika.
NHC yatoa
kauli
SHIRIKA la Nyumba la
Taifa (NHC) limesema kuwa mbia wao alikuwa na vibali vya mamlaka zinazohusika
kusimamia ujenzi wa majengo makubwa vya kumruhusu kuongeza ghorofa 16 kutoka
kumi za awali.
Kauli hiyo inakuja
kukiwepo na mvutano kutoka mamlaka mbalimbali ikiwemo Manispaa ya Ilala kwamba
mbia wao huyo ambaye ni M/s Ladha Construction alipewa kibali cha kujenga
ghorofa kumi, lakini cha kushangaza aliongeza nyingine sita bila taarifa na
hivyo kusadikiwa kuwa huenda ndiyo chanzo cha kuanguka kwa jengo
hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa
NHC, Nehemiah Mchechu akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaa, alisema Agosti 22 mwaka jana mbia wao huyo aliwataarifu kuwa ameshapata
vibali kutoka mamlaka husika, na kwamba angependa aingie nao mkataba mdogo
kutambua ongezeko la ghorofa hizo na mabadiliko ya tarehe ya kumaliza
mradi.
“Shirika lilimjibu kuwa
hakuna pingamizi kama mbia ataleta nakala ya vibali kutoka mamlaka husika kwa
ajili ya kumbukumbu za shirika na pia ili kufikia hatua za maamuzi ya ndani na
mawasiliano yote hayo yapo kwenye rekodi zetu na endapo mamlaka husika
itazihitaji tuzazipatia,” alisema.
Kutokana na hali hiyo,
aliutaka umma kutoliingiza shirika hilo katika sakata hilo kwa madai kuwa zipo
taasisi na vyombo vinavyokasimiwa mamlaka ya kusimamia ubora wa ujenzi wa nyumba
nchini, na NHC nayo husimamiwa na taasisi na vyombo hivyo.SHUKRANI TANZANIA
DAIMA
Post a Comment