IMEELEZWA kuwa, mtuhumiwa Omar
Mussa Makame (35) anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kumuua Padri
Evaristus Mushi ni mwanachama wa CUF ambaye aligombea nafasi ya uwakilishi
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 katika Jimbo la Rahaleo kwa tiketi ya Chama
cha Wananchi (CUF).
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Hamad Masoud alithibitisha jana kuwa, mtuhumiwa huyo ni mwanachama wao na
alishiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu na kusimamishwa na chama katika
kampeni za Uwakilishi Jimbo la Rahaleo.
“Ni kweli mtuhumiwa
anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Padri Mushi ni
mwanachama wetu na alishiriki katika mchakato wa kuwania Uwakilishi Jimbo la
Rahaleo mwaka 2010.
Hata
hivyo, Hamad alisisitiza na kusema suala la Omar kamwe lisihusishwe na CUF na
kusema suala hilo watalitolea tamko baadaye.
Kwa
mujibu wa kumbukumbu za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ripoti ya matokeo ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 Jimbo la Rahaleo, mgombea wa CCM, Nassor Salim Ali
maarufu kama Jazirra aliibuka na ushindi kwa kupata kura 3,952 sawa na asilimia
63.10, wakati mgombea wa CUF, Omar Mussa Makame alipata kura 2,310 sawa na
asilimia 39.9 na kushika nafasi ya pili.
Taarifa
iliyotolewa na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mussa Ali Mussa mtuhumiwa
anatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Kukamatwa kwa Omar kunatokana na michoro
ya teknolojia ya kisasa chini ya msaada wa upelelezi wa makachero kutoka FBI
ambayo iliweza kutambua sura yake.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili
umegundua kwamba mtuhumiwa huyo licha ya kuwa mfuasi wa CUF, mama yake mzazi ni
kada wa CCM.
Mama
yake, Tatu Sheha mkazi wa Mkele, Unguja ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi
wa CCM katika Jimbo la Kwamtipura.
Tangu
kuibuka kwa kadhia hiyo inayomhusu mtoto wake, mama mzazi amekosa raha na faraja
kiasi ya kushindwa kuhudhuria vikao vya chama kwa takribani wiki mbili
sasa.
Baadhi
ya wananchi Zanzibar wamepongeza juhudi za Jeshi la Polisi za kufanikisha
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, wakisema ni dalili njema za kutaka kukomesha
matukio ya mauaji kisiwani
Zanzibar.
Post a Comment