Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mary Lugola akihutubia wananchi wakati wa siku ya
maadhimisho ya Mtoto wa Mtaani iliyofanyika tarehe 12/04/2013 katika uwanja wa
Sheikh Amri Abeid uliopo mjini Arusha. -1.JPG)
Baadhi ya wanafunzi wa shule
ya Msingi mojawapo iliyopo Mkoani Arusha wakiwa wanashiriki mashindano ya
kukimbia kwa kutumia magunia yaliyofanyika mapema katika siku ya kuadhimisha
Mtoto wa Mtaani iliyofanyika tarehe 12/04/2013 kwenye uwanja wa Sheikh Amri
Abeid mjini Arusha. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi.
Na Rashid
Nchimbi, Arusha.
JESHI la Polisi Mkoani
hapa limesema litaendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kulinda na
kutetea haki za watoto.
Hayo yalisemwa na
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mary Lugola ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha
Polisi Jamii Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya
siku ya mtoto wa mtaani duniani.
Katika maadhimisho hayo
ambayo yalifanyika tarehe 12 mwezi huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini
hapa, Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi alisema kwamba jeshi la polisi kupitia
dawati la jinsia na watoto mkoani hapa limekuwa karibu sana kiutendaji na
mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya serikali kama vile Mkombozi, CCR, Action For
Children n.k katika kutetea na kulinda haki za watoto wa
mitaani.
Mrakibu huyo Mwandamizi
wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha alisema
mbali na jeshi hilo kujihusisha katika kutetea na kulinda haki za watoto wa
jamii hiyo, pia linasaidia kuinua na kuibua vipaji vya watoto hao kupitia
programu ya MWONGORIKA ya Polisi jamii ambayo inajihusisha na michezo kwa
vijana.
Alisema kupitia Dawati
hilo, jeshi la polisi limeweza kuwahudumia watoto wa mitaani kwa kushirikiana na
mashirika hayo ili kuwawezesha waishi katika mazingira salama na kupata mahitaji
muhimu.
“Kwa
mfano tumeshawahi kuwaunganisha na wazazi wao pamoja na kuwasafirisha kwenda
makwao watoto waliokuwa tayari kurudi ”. Alisema Bi. Lugola.
Alimalizia kwa kusema
kwamba Dawati la Jinsia na watoto huwa linahakikisha linapata taarifa za watoto
walioathirika na pia wale wote wanaowanyanyasa watoto hao wanachukuliwa hatua za
kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Nalo shirika la
Mkombozi kupitia risala yao iliyosomwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Shirika hilo
Bi. Doris Cornell alisema kwamba ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku
hiyo ni “Nyumbani Mtaani Nyumbani” ikiwa na maana ya kwamba, mtoto atatoka
nyumbani kwenda mtaani na kisha atarudi nyumbani.
Alisema lengo la siku
hiyo ni kuwapa jukwaa watoto waishio na kufanya kazi mtaani wakiungana na
wengine duniani kote kupaza sauti ili haki zao zisiipuzwe.
Bi. Doris alisema
watoto waishio mitaani na kulala mitaani wanazofursa na haki sawa na watoto
wengine duniani na kwamba wana haki ya kuishi, kulindwa, kuendelea na kushiriki
katika mambo yanayogusa maisha yao kama ilivyoainishwa katika mkataba wa
Kimataifa wa haki za watoto kifungu cha 4.
Risala hiyo ilieleza
sababu za kuwepo kwa watoto hao mitaani ni pamoja na kukosa haki za msingi
(chakula, malazi, mavazi, ulinzi, elimu, upendo, matibabu n.k) kutoka katika
familia zao, kufiwa na mzazi mmoja au wote wawili, Sababu nyingine ni vitendo
vya unyanyasaji na ukatili waliofanyiwa katika jamii au familia, kipato duni
katika familia/wazazi/walezi, utumikishwaji wa watoto (ajira za watoto),
kubaguliwa na kunyang’anywa mali za wazazi wao.
Siku hiyo ambayo huwa
inaadhimishwa katika nchi 130 duniani, Tanzania na Uingereza ikiwa ni miongoni
mwa nchi hizo, ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya pamoja
na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi
Maria Maswa.


Post a Comment