DODOMA.
*******
SERIKALI ya Rais Jakaya
Kikwete imelaumiwa kwa kutenga Sh1 bilioni kwa ajili ya maziko ya viongozi huku
Watanzania wengi wakilia na umaskini mkubwa.
Shutuma hizo zilitolewa
mwishoni mwa wiki bungeni kwa nyakati tofauti wabunge akiwamo wa Viti Maalumu
Lucy Owenya (Chadema) na Kangi Lugola (Mwibara-CCM) wakati wakichangia hotuba ya
makadirio ya bajeti katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha
2013/14.
Katika mchango wake
Owenya alisema inatia aibu kuona kiasi kikubwa cha fedha kikitengwa kwa ajili ya
maandalizi ya kuzika viongozi huku mambo muhimu na ambayo ni kipaumbele
yakiachwa.
“Ni aibu na fedheha
kubwa, hivi mmetenga kiasi hicho kwani mnajua nani atakufa na lini atakufa ndio
maana mnajiandaa kumzika,” alihoji Owenya.
Mbunge huyo alikwenda
mbele zaidi na kueleza kuwa Serikali imeshindwa kufikiri na hasa namna ya
kuwaondolea umasikini na tabu wanazopata wananchi wake lakini inawaza habari za
watu wanaojiandaa kufa.
Vile vile katika mchango
wake Lugola ambaye alisema asingeunga mkono hotuba ya makadirio ya mapato na
matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alihoji sababu za kutengwa kwa fedha hizo bila
kujua nani atakufa lini.
Mbali na hilo, Owenya
pia aliilaumu Ofisi ya Waziri kwa kushindwa kutumia mbinu mbadala za kuzuia
matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi zinazotumiwa na wakuu wa mikoa kwa
ajili ya kwenda Dodoma kufuatilia hotuba ya Waziri Mkuu.
Alimtaka Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kuwatimua wakuu wa mikoa ili warudi mikoani kwao ili kuokoa fedha
za walipa kodi zinazoteketea katika misafara yao mjini Dodoma.


Post a Comment