Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (pichani) ameanza mchakato wa kuunda serikali mpya ambapo ametangaza majina ya mawaziri wanne.
Wanne hao ni pamoja na Dkt. Fred Okeng’o Matiangi ambaye atakuwa ni Waziri Mteule wa Teknolojia na Mawasiliano, Henery Rotich aliyemteua kuwa Kuwa waziri wa Fedha, James Wanaina Macharia aliyekabidhiwa Wizara ya Afya na Balozi Amina Mohammed ametangazwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Ilitarajiwa kwamba Rais Kenyatta angewataja mawaziri wote 18, lakini amesema wengine watatangazwa baadaye na kuomba taifa kuwa na subira.
Wakati huo huo Bunge la Kenya limeidhinisha kamati maalum inayoongozwa na Spika wa Bunge Justin Muturi ambayo itawachuja mawaziri watakaoteuliwa na Rais.
Chini ya katiba ya Kenya bungelina mamlaka ya kupitisha majina ya maafisa wakuu wa serikali, wakiwemo Mawaziri, mabalozi na wakuu wa tume za kikatiba.