Na Boniface Wambura,TFF
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayofanyika Julai mwaka huu nchini Zambia.
Taifa Stars inashiriki michuano hiyo ya timu za Taifa za nchi wanachama wa COSAFA ikiwa timu mwalikwa. Nchi wanachama wa COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoro, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Michuano hiyo itafanyika kuanzia Julai 6 hadi 21 mwaka huu katika miji ya Lusaka, Ndola na Kabwe. Ratiba ya makundi ya michuano hiyo itapangwa Mei 3 mwaka huu jijini Lusaka.
Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika miaka mitatu iliyopita. Hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo baada ya kucheza ya kwanza iliyofanyika mwaka 1996 nchini Zimbabwe.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inatarajia kuingia kambini mwishoni mwa mwezi ujao kujiandaa kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.
Juni 16 mwaka huu Taifa Stars itacheza na Ivory Coast jijini Dar es Salaam katika mechi nyingine ya mchujo ya Kombe la Dunia wakati Juni mwishoni na Julai mwanzoni itacheza mechi ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Uganda.
Wakati huo huo, waandishi wa habari wanaotaka kuripoti michuano hiyo wanatakiwa kuwasilisha majina yao TFF kabla ya Aprili 27 mwaka huu ili maombi yao yatumwe COSAFA kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho (Accreditation).
Post a Comment