ofisa wa Upelelezi Mbozi akionyesha sehemu ya Mbolea
mbovu ambayo imefumbiwa macho na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania na
kuitakatisha kama haina matatizo wala madhara kwa wakulima
***********
Katika hali inayoonyesha kuna mchezo mchafu wa kuendelea
kuwamaliza wakulima wilayani Mbozi, shehena ya Mbolea mbovu iliyozuiwa kuuzwa
mwaka jana hatimaye “upepo umepita” na kuruhusu iendelee kuuzwa kwamba ipo juu
kiviwango!
Katika hali hiyo wakulima wamekuja juu jana wakati
wakishuhudia ufunguzi wa duka la STACCO ambalo miezi kadhaa lilishuhudiwa likiwa
limepigwa makufuli na kwa mbwembwe nyingi ikiwemo msururu wa vyombo vya habari,
lakini kwa jana ilikuwa kimya kimya kufuli la kwanza likafunguliwa, likafuata la
pili na hatimaye la tatu!
Wakati wananchi kwa macho yao meupe wakishuhudia mifuko
iliyoganda ya Mbolea za UREA, DAP, CAN na SA taarifa iliyotolewa kuruhusu
kufunguliwa kwa duka hilo inatoa maelezo kuwa ni Mbolea ya SA peke yake ndiyo
iliyobainika kuwa na ubora hafifu! ambayo ni mifuko 11
tu.
Hata hivyo afisa anayesimamia ubora wa Mbolea katika
halmashauri ya wilaya ya Mbozi Bi Shonyela amesema licha ya maelekezo kutoka juu
mengine hayatatekelezeka kwani kufanya hivyo itakuwa ni kuwamaliza wakuliwa wa
wilaya yake kwakuzingatia kuwa Mbolea iliyoganda kuto kufaa tena
mashambani.
“nimeandikiwa Mbolea aina ya SA pekee ndiyo isafirishwe
chini ya usimamizi wa polisi kwenda Dar es Salaam lakini ni mifuko 11tu! Wakati
kuna mbolea aina nyingine ambazo ni zaidi ya mifuko 50 hazina viwango vya ubora
na taarifa imekuwa kimya” alifafanua
Uchunguzi wa haraka kwenye duka hilo unaonyesha kuwa
mifuko16 ya DAP ilikuwa imeganda wakati wa kufunga duka hilo mwezi September
mwaka jana, UREA mifuko 16, CAN 11 na SA 11.
Ingawa katika maelezo ya mkurugenzi wa Mamlaka ya
udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA ilionyesha kuwa wangeshirikiana bega kwa bega
na TBS katika kuhakikisha viwango vya bidhaa hiyo vinasimamiwa, maamuzi ya
kuruhusu uuzwaji wa mbolea aina ya DAP, CAN na UREA iliyoharibika kwenye ghala
la STACO wilayani Mbozi yanajenga mawimbi na mashaka kwa wananchi kuwa mamlaka
imelainishwa na ama wamefumbishwa macho!
Tanzania hutegemea maabara yake ya Mbolea iliyopo
Mlingano mkoani Tanga kuthibitisha ubora wa bidhaa hizo hata hivyo kumekuwepo
udanganyifu unaofanywa na baadhi ya maofisa wa serikali na kuwasaliti wakulima
kutokana na makampuni yanayofanya shughuli za usambazaji wa pembejeo na hasa
Mbolea kushika keki kubwa katika mzunguko wa fedha
nchini
Wakati pia chuo cha kilimo SUA kimekuwa kikitumika katika
tafiti na uchunguzi wa Mbolea, mwaka jana Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika Dr
Adam Malima alikataa matokeo ya uchunguzi wa mbolea yaliyotolewa na SUA na
kuahidi sampuli za Mbolea iliyokamatwa RUVUMA kupelekwa nchini Afrika kusini
kujiridhisha na uchuguzi wa maabara za huko baada ya kulalamikiwa na
wakulima
Aidha naibu waziri alisitisha leseni za makampuni ya
STACO na Mohamed Enterpries mnamo August 07 mwaka jana, ambapo baada ya siku
kadhaa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania Suzana Ikelya alitua
Mbozi na kukamata Mbolea kwenye duka la STACO
“Maamuzi ya mamlaka ya ukaguzi wa ubora wa Mbolea
yanawaacha wananchi wilayani Mbozi wakikosa imani kutokana na namna maamuzi
yanavyofikiwa hata katika mambo ambayo hayahitaji utaalamu kuthibitisha ubora
kama suala la Mbolea iliyoganda” anaeleza bwana Keneth Mwazembe mmoja wa
wakulima wakubwa wilayani Mbozi.
Msimamizi wa duka la STACO bwana Julius Masai licha ya
kufurahia kufunguliwa kwa ofisi yake ya chakula, amesema ni kweli kwamba kuna
mbolea ambayo haimo kwenye barua ya kuruhusu uuzwaji ambayo haifai kwa matumizi
lakini wanatumia busara kuitenga licha ya kutoelezwa kwenye barua
hiyo
Ni kweli kuna mifuko kama 37 hivi ya mbolea mchanganyiko
ambayo ni mbovu na tumeitenga pembeni na hatutaiuza” alisema meneja huyo bwana
Julius Masai
Duka hilo limefunguliwa jana chini ya usimamizi wa
maofisa wawili wa idara ya upelelezi ya jeshi la polisi na ofisa anayesimamia
ubora wa MBOLEA wilaya ya Mbozi, na shughuli hiyo imefanyika kimya kimya tofauti
na mbwembwe zilizofanyika wakati wa kufunga duka hilo ambapo wananchi waliokuwa
wakipita barabarani waliitwa kushuhudia namna
wanavyotendwa!
Kwahisani ya Indaba Africa
|
Post a Comment