Mkazi
Wa Mburahati Jogoo jijini Dar es salaam, Nassor Issa Mohamed (25)
amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja au kulipa faini ya shilingi milioni
tatu kwa kosa la kuwatumia ujumbe wenye nia mbaya wa simu ya mkononi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi na Inspekta
General wa Polisi Said Mwema.
Akitoa
hukumu hiyo hakimu Helen Riwa wa mahakama Kisutu aliiambia mahakama kuwa
Mohamed alisajili kadi zake za simu kwa majina tofauti na kwa mitandao
tofauti kwa nia ya kutumia kadi hizo kutuma ujumbe wa simu wenye nia
mbaya kwa viongozi hao.
Alisema
mshtakiwa alikutwa akiwa na kadi ya simu yenye namba 0759 799956 ya
Vodacom iliyosajiliwa kwa jina la Fadhil Issah, nyingine ya Airtel 0687
521948 iliyosajiliwa kwa jina la Godfrey Joseph na kadi yenye namba
0687521947 ya Airtel iliyosajiliwa kwa jina la Fadhil Issa.
Hakimu
Riwa aliitaka jamii kutumia kwa uangalifu mitandao kwa kuwa ni
teknolojia mpya ambapo makosa yake yanakuwa ni mapya na sheria ni mpya.
Alisema ametoa adhabu hiyo kwa kutumia Sheria ya Mawasiliano ya
kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 kifungu cha 132 ili iwe
fundisho kwa wote wenye nia ya kufanya makosa kama hayo.
Awali
Mwendesha Mashitaka Ladislaus Komanya aliiambia mahakama kuwa mnamo Mei
20 mwaka huu taarifa za kiinteligensia zilifikishwa kwa Maafisa wa juu
wa jeshi la Polisi kuwa kuna mtu aliyesajili simu zake kwa mitandao
tofauti anatumia simu hizo kuwatumia ujumbe mbaya wa simu ya mkononi
Waziri Nchimbi na IGP na baada ya upelelezi ilipobainika kuwa namba hizo
zilikuwa zimesajiliwa kwa majina tofauti.
Alisema iligundulika kuwa namba hizo zilikuwa zinamilikiwa na mtu huyo ambaye jina lake halisi ni Nassor Issah Mohamed
Alisema
Mohamed alikamatwa Mei 25mwaka huu na baada ya mahojiano alikiri
kumiliki kadi ya simu na kwamba ndiyo yeye aliyesajili namba hizo kwa
mitandao tofauti akitumia majina tofauti ili kuficha utambulisho wake
akiwa na lengo lakufanya uhalifu. Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa
mara ya kwanza Mei 27 mwaka huu na kukiri mashitaka.
Post a Comment