Mheshimiwa
Zitto Kabwe akikabidhi barua kwa Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania
Dianna Melrose inayokwenda kwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.Picha na Chadema
--
Waziri
Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
kupitia Chadema, amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Cameron akimwomba kufuta sheria ya nchi yake inayowalinda watoroshaji wa
fedha za umma wa nchi mbalimbali.
Zitto pia
amemwomba Cameron kuzishawishi nchi nyingine tajiri kuwa na sheria za
aina hiyo ili kudhibiti mafisadi wa nchi zinazoendelea.
Hatua hiyo
ya Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Tanzania
Bara, ni mwendelezo wa juhudi zake za kupambana na mafisadi ndani ya
Serikali wanaodaiwa kuweka katika benki za nje kiasi cha dola za
Marekani milioni 196 (sawa na Sh323 bilioni).
Zitto
amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia kuwa Waziri Mkuu Cameron atakuwa
mwenyeji wa Kundi la Nchi Tajiri Duniani linalojulikana kama G-8 ambalo
litakutana Lough Erne, Uingereza kuanzia Juni 17–18. Cameron ndiye
atakuwa Mwenyekiti wa mkutano huo.
Novemba
mwaka jana, Mbunge huyo alipeleka hoja binafsi bungeni akitaka iundwe
timu maalumu kwa ajili ya kufuatilia kiasi cha Sh 323 bilioni ambazo
zimethibitika kufichwa Uswisi.
Zitto
aliikabidhi barua hiyo Jumatatu ya wiki hii kwa Balozi wa Uingereza
nchini Dianna Melrose, akimwomba aiwasilishe kwa Waziri Mkuu Cameron,
kuelezea kilio cha Watanzania kuhusiana na fedha hizo.
Alisema
sheria hiyo ina athari kubwa kwa maisha ya Watanzania wengi maskini na
Afrika kwa ujumla, ambapo alisema anaamini sheria inayotaka uwazi
itapitishwa kwenye mkutano wa mataifa manane tajiri yenye viwanda
duniani, maarufu G-8, utakaofanyika mwezi ujao.
Akizungumzia
suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alisema
kuwa ana taarifa kuhusu barua hiyo iliyoandikwa na Zitto kwenda kwa
Cameron kuhusu shinikizo la Serikali kufanya mchakato wa kurudisha fedha
zilizofichwa nje ya nchi.
“Tunafanya
kazi na siyo kuzungumza ovyo kila mahali au kila hatua tuliyofikia, ila
tunafanya kazi masaa yote, Watanzania wasubiri tu hatua tutakayofikia na
tukiona tumejiridhisha tutawaambia nini kimefanyika,” aliongeza Werema.
Post a Comment