Simu ya mkononi iliyolowa
maji.
Kuna wakati katika shughuli
za kawaida inatokea kwa bahati mbaya simu ya mkononi inatumbukia kwenye
maji na kulowa au hata kumwagikiwa na kimiminika cha aina yeyote labda chai,
juisi, kahawa, soda nakadhalika lakini napenda kuzungumzia maji kama mfano
mzuri. Unaweza kujiepusha na hili lakini kwa kuwa kulowa hutokea kama ajali basi
ikiwa simu yako ya mkononi imetumbukia kwenye maji na kulowa, fanya
yafuatayo:
Hatua.
Zima simu yako baada ya
kulowa au kutumbukia kwenye maji kama haikuzima yenyewe. Toa mfuniko wa betri
na betri. Toa kadi ya simu, kisha kwa uangalifu toa mfuniko
wa kicharazio na kicharazio (keypad). Baada ya haya chukua kipande
cha godoro ama kitambaa kisichotoa na kuacha nyuzinyuzi kwa urahisi na pangusa
taratibu sehemu za simu yako ili kunyonya maji yaliyolowesha. Ukimaliza zoezi
hili unaweza kuanika sehemu za simu yako iliyolowa juani ama ukaziweka sehemu za
simu yako juu ya mchele mkavu (ambao haujapikwa). Mchele utafyonza unyevunyevu
wote. Unaweza kufanya haya kwa muda wa dakika ishirini hivi.Kisha kama
utajiridhisha kwa kuona simu yako imekauka vizuri kabisa rudishia kila kitu cha
kwenye simu yako vizuri ikiwemo betri, kicharazio (keypad) na kifuniko cha betri
na jaribu kuwasha.
Kama simu yako haikupata
hitilafu kubwa ilipolowa uwezekano wa simu yako kuwaka ni mkubwa lakini pia kama
haitawaka ni vyema ukamuona fundi simu kwa matengezo zaidi
Laptop iliyolowa
maji.
Wakati mwingine pia laptop
inaweza kumwagikiwa na kimiminika chochote lakini napenda kuzungumzia maji kama
mfano, maji yanapomwagikia kwenye laptop yako ni afadhali kuliko kimiminika
kingine kinachonata kama soda, uji au juisi. Kama tunavyojua maji ni mepesi na
ni rahisi kitiririka kwa urahisi kuliko vimiminika vingine vizito vyenye kunata.
Kompyuta (laptop) yako inapomwagikiwa na maji sehemu zinazoathirika zaidi ni
zile zenye upenyo wa kuwezesha maji kupenya kama keyboard, port za USB, HDMI
nakadhalika. Unachotakiwa kufanya ni kama ifuatavyo.
Hatua.
1. Kama baada
ya laptop yako kumwagikiwa na maji haikuzima yenyewe basi izime.
2. Chomoa
vifaa vyovyote ulivyochomeka kwenye port za laptop.
-Ikishazima laptop toa
betri, chomoa adapter cable kama ulikuwa ukichaji laptop na ondoa vifaa vyovyote
ulivyochomeka kwenye port za laptop kama USB flash disk, external hard
disk au external CD/DVD ROM. Utafanya hivyo ili kuepusha shoti
kwasabu maji yakishaingia kwenye vyanzo vya umeme husababisha shoti na hitilafu
kubwa itakayoleta athari kwa vifaa vingine kwenye laptop.
3. Igeuze
laptop yako juu chini ili maji yaliloingia kwenye laptop yaweze kutiririka na
kuepusha maji kuingia ndani zaidi kwenye mashine yako.
4. Kausha
sehemu yoyote unayoweza kukausha kwenye laptop yako kwa kutumia kitambaa laini
kinachokausha vizuri bila kuacha nyuzinyuzi.
5. Kama
unaujuzi wa kutengeneza kompyuta, unaweza kuifungua laptop na kusambaratisha
baadhi ya sehemu za laptop kama keyboard, cards na hard disk
drive kisha futa kwa utaratibu na uhakikishe sehemu zote zilizoingiliwa na
maji unazikausha bila kuacha unyevu unyevu. Kama kuna uchavu au mnato wowote
ufute ikiwezekana tumia brashi kama mswaki kusafisha ili kuepusha mgusano
utakaosababisha shoti.
ANGALIZO: Kama huna ujuzi wowote wa kutengeneza komyuta
(laptop) usithubutu kuifungua ni vyema ukapeleka kwa fundi au kumpa mtu mwenye
ujuzi akusaidie.
Unashauriwa baada ya kufuta
laptop yako vizuri acha kwa muda wa saa 24 mpaka saa 48 ili uwe na uhakika
imekauka vizuri kabisa. Kama laptop yako ilimwagikiwa na maji kidogo basi heri
zaidi angalau iache kwa saa 12 kisha rudishia vifaa vyote ulivyosambaratisha kwa
kuvifunga vizuri na jaribu kuwasha.
Kama laptop yako haitawaka
basi ipeleke kwa fundi wa kompyuta kwa matengenezo zaidi.
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana
na mada hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!
Post a Comment