Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dr. Fenella Mukangara.
|**********
Serikali
imesikitishwa na taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mtanzania Jumapili
ukurasa wa 19 toleo namba 7327 la tarehe 26 Mei mwaka huu yenye kichwa
cha “DR. MUKANGARA ANA ROHO NGUMU HAJALI KITU” na ile ya gazeti la Rai la Alhamisi 30 Mei 2013 yote ya Kampuni ya New Habari (2006) Limited inayosema “ YA MUKANGARA YASIACHWE YAKAPITA”.
Taarifa
hizo hazina ukweli na waandishi wa maoni hayo wanaonekana kutaka
kumchonganisha Waziri na wananchi kwa kuandika mambo ambayo hayana
ukweli na yenye dhamira ya kumchafua Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo Dr. Fenella Mukangara .
Ikumbukwe
kwamba wakati Said Kubenea akimwagiwa tindikali na Ndimara Tigambwage
akiumizwa na majambazi ilikuwa mwaka 2008 wakati huo Waziri Mukangara
hakuwa Waziri wala hakuwa Mbunge .
Kadhalika
mwandishi wa habari Richard Masatu alifariki huko Mwanza mwaka 2011,
Waziri Mukangara alikuwa Naibu Waziri chini Dr. Emmanuel Nchimbi.
Masuala ya
waandishi wa habari kuuawa na kuumizwa yako katika vyombo vya sheria
hivyo basi si sahihi kwa Waziri wa Habari kutoa kali kabla ya vyombo
husika havijamaliza kazi zake. Mara baada ya vyombo hivyo kumaliza kazi
yao Wizara itakuwa na cha kuwaambia wananchi.
Vile vile
ikumbukwe kwamba Serikali hufanya kazi kama kitu kimoja wakati wa
utekelezaji wa majukumu yao mbalimbali ambayo yaweza kuingilia toka
Wizara moja hadi nyingine , hivyo baada ya kutokea kwa kifo cha David
Mwangosi waandishi wa habari waliandamana hadi Jangwani ambapo Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi Dr. Emmanuel Nchimbi alikwenda viwanja vya
Jangwani kutoa pole kwa Waandishi wa habari kufuatia kifo hicho kwa
niaba ya Serikali lakini waandishi walikataa uwepo wake katika kusanyiko
lile.
Hatua ya
wanahabari waliokuwa wamekusanyika Jangwani kumkataa Waziri Nchimbi
ilisababisha Serikali kushindwa kutoa pole zao ambapo zingejumuisha
Serikali na wadau wote.
Kwa hiyo
tunawaomba waandishi wa habari wanapoandika maoni au makala ni vema
wakawasiliana na wahusika au wanaowashutumu ili nao wapate fursa ya
kujitetea na sio kuwalisha mawazo ambayo hawakuwa nayo.
Aidha,waandishi
wa maoni wasilazimishe matakwa na maoni yao binafsi yaonekane kuwa
sahihi na hivyo Serikali lazima ifanye wanavyotaka wao na ni vyema
wangepata muda wakamhoji Waziri mwenye dhamana ya habari wakapata ukweli
kuliko wao kumuhukumu Waziri kwa kuwa tu wahariri wao wamewapa nafasi
katika magazeti yao kuandika maoni yao ambayo ni potofu na yanataka
kujenga chuki dhidi ya waziri mbele ya jamii
Vile vile
ni jukumu la Waziri kuzisemea sekta za habari,Vijana,Utamaduni na
Michezo zikiwemo Taasisi zote zilizopo katika sekta hizo na si
vinginevyo.
Inashangaza
kuona mwandishi wa maoni katika gazeti la Mtanzania Jumapili akihoji
Waziri kuzungumzia sekta ya habari, vijana , utamaduni na michezo na
Taasisi kama vile Shirika la Utangazaji na mbio za Uhuru na kuziita ni
porojo.
Watoamaoni
wameshindwa hata kuona mambo mazuri yaliyomo katika Kitabu cha Bajeti ya
2013/14 ikiwemo kuleta Bunge muswada wa uanzishwaji wa Baraza la Vijana
, na Muswada wa kusimamia vyombo vya habari kwa ajili ya kuboresha
maslahi na utendaji wa wanahabari ikiwemo kuwa na Bima wanapokuwa katika
kazi hatarishi.
Hata hivyo
Mheshimiwa Waziri anahuzunisha na vitendo vya kikatili ambavyo
wanavyofanyiwa waandishi wa habari na hivyo kutoa wito kwa wananchi
kuviachia vyombo vya usalama viendelee kufanya kazi yake .
Kwa ujumla
taarifa hizo zimemhuzunisha Mh. Waziri kwa kuwa amekuwa akishirikiana na
anaendelea kushirikiana bila kuchoka na waandishi wa habari katika
shughuli mbalimbali ziwe za raha na huzuni.
Post a Comment