Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana ana Wanafunzi wa
Skuli ya Msingi wa Miwani, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa jengo lao
jipya. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akilizindua rasmi
jengo jipya la madarasa mawili ya Skuli ya Msingi ya Miwani iliyomo
ndani ya Jimbo la Uzini.
Mwakilishi
wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza akimpatia maelezo ya ujenzi wa Jengo la
Skuli ya Msingi ya Miwani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif mara baada ya kulizindua rasmi.
Balozi
Seif akimpongeza Msaidizi Mkurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar {
PBZ } Ame Haji Makame kwa hatua ya benki hiyo kusaidia vikalio kwenye
jengo jipya la skuli ya msingi ya miwani. Kulia
yao ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Mohd Raza Hassan na Pembeni yao
Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Dr. Islamu Idriss.
*********************************
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati
umefika kwa Wananchi kuwa na hadhari katika kuangalia Mtu mwenye
muelekeo wa kuwafaa katika kuwasimamia kusukuma mbele maendeleo yao
wanayoyahitaji kwenye maeneo yao.
Kauli
hiyo aliitoa wakati akizindua rasmi jengo jipya na la kisasa la Skuli
ya Msingi ya Miwani ndani ya Jimbo la Uzini lililojengwa ndani ya
kipindi cha miezi miwili na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd Raza
Hassan.
Balozi
Seif alisema ile tabia ya baadhi ya wananchi kukumbatia watu
wanaoendeleza ubinafsi inafaa kupigwa vita kwa hali yoyote ile kwa vile
inachangia kuzorotesha kasi ya Maendeleo ya Wananachi.
Aliwahimiza
Viongozi, washirika na wahisani zikiwemo Taasisi za Kijamii na zile za
maendeleo zilizomo katika Halmashauri za Wilaya kujikita zaidi katika
kuunga mkono juhudi za Wananachi kwenye sekta za Mendeleo na Kiuchumi
wakiangalia zaidi ile sekta muhimu ya Elimu.
“
Siku zote tunasema tuwekeze kwenye elimu ambayo watoto wetu itawasaidia
wao wenyewe kwa kupata muelekeo na mafanikio ya maisha yao sambamba na
kusaidia familia zinazowazunguuka “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini
Mh. Mohd Raza kwa hatua yake aliyochukuwa ya ujenzi wa Jengo hilo la
madarasa mawili lililokamilika huduma zote ikiwemo vikalio ambalo
limesaidia kuiepusha Skuli ya Miwani kuchukuwa wanafunzi katika mikondo
miwili.
Balozi
Seif alisema juhudi za Mwakilishi huyo ni miongoni mwa utekelezaji wa
ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ya CCM pamoja na kukamilisha ahadi
alizotowa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo hilo.
Aliwakumbusha
Viongozi wengine wa Jimbo, Wilaya na hata mkoa kuunga mkono jitihada za
Wananachi wa Miwani katika kukamilisha jengo jengine la Madarasa Sita
la Skuli hiyo ambalo linahitaji nguvu za ziada za Viongozi hao likiwa
limekwama kwa miaka minne sasa.
Alisema
katika kuunga mkono juhudi hizo za Wananchi ambapo zinahitajika kiasi
cha shilingi Milioni Tisa { 9,000,000/- } kukamilisha hatua ya linta ili
likabidhiwe Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa Ukamilishaji
aliahidi kuchangia Shilingi Milioni Mbili { 2,000,000/- }.
“
Sisi viongozi kuanzia Wawakilishi wa kuteuliwa, Mbunge, Madiwani na
hata halmashauri za Wilaya tunalazimika kuunga mkono juhudi hizi ili
kutowavunja moyo wananchi tunaowaongoza katika Majimbo yetu “.
Alikumbusha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa
salamu za Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } iliyosaidia Vikalio vyote
vya jengo hilo Meza 100 na Viti 100 vyenye thamani ya shilingi Milioni
16,000,000/- Msaidizi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Ame Haji
Makame amesema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Wananchi
popote pale.
Nd.
Ame alisema benki ya Watu wa Zanzibar inajali maendeleo ya Jamii na
wakati mwengine kushawishika kusaidia miradi yao tofauti ikiwemo zaidi
sekta ya elimu ambayo ndio mkombozi wa Taifa lolote.
Naye
kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar Bibi Mwanaidi Saleh amempongeza Mwakilishi wa Jimbo la Uzini
Mh. Raza kwa juhudi zake za kusaidia nguvu za Wizara hiyo katika
ukamilishaji wa majengo ya Skuli.
Bibi
Mwanaidi alisema juhudi za Mwakilishi huyo za kukamilisha majengo
mawili ya Skuli ndani ya Jimbo hilo limeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya
Elimu wa kukamilisha majengo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na
wizara hiyo.
Katibu
Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu amewakumbusha Wananchi katika maeneo mbali
mbali Nchini kuhakikisha kwamba majengo ya skuli wanayoyaanzisha
yanatengewa vyumba maalum kwa ajili ya vitengo vya Kompyuta.
Alisema
Wizara imeanzisha mfumo maalum wa mafunzo ya kompyuta kuanzia elimu ya
msingi kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa Zanzibar kwenda sambamba na
mabadiliko ya sayansi na Teknolojia yaliyopo Duniani.
Akitoa
shukrani zake katika hafla hiyo ya uzinduzi wa jengo jipya la Skuli ya
Miwani iliyomo ndani ya Jimbo la Uzini Mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Mohd
Raza Hassan alisema kwamba uwepo wa Viongozi katika Jamii upo kwa ajili
ya kusimamia matakwa ya Wananchi.
Mh.
Raza alisema tabia ya baadhi ya Viongozi kuigonganisha vichwa jamii ni
kutowafanyia haki Wananachi wanaowaongoza na hatimae inaviza maendeleo
yao na kuwaongezea chuki na fitna baina yao.
Mapema
katika Risala yao iliyosomwa na Mwalimu wa Skuli ya Msingi ya Miwani
Juma Abdulla wananchi hao wa Kijiji cha Miwani walisema bado
wanakabiliwa na changamoto kadhaa ndani ya Kijiji hicho.
Mwalimu
Juma alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa bara bara,
mashine za uchapaji , ukosefu wa Daktari katika kituo chao cha Afya
pamoja na umaliziaji wa jengo lao la madarasa sita ambalo linaweza
kusaidia muendelezo wa mkondo mmoja tu skulini hapo.
Jengo
jipya la madarasa mawili la Skuli ya Msingi ya Miwani litakalokuwa na
uwezo wa kuchukuwa wanafunzi 122 ambapo wanafunzi 56 kwa kila
chumba lilijengwa ndani ya kipindi cha miezi miwili kwa gharama za
shilingi Milioni 30,000,000/- .
Katika
hafla hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Uzini pia alikabidhi Mchango wa
Shilingi Milioni Mbili kwa ajili ya Kusaidia maandalizi ya Sherehe za
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi Mtukufu ya Zanzibar hapo mwaka
2014.
Fedha
hizo zitasaidia katika Ofisi ya Mkoa Kusini Unguja, Wilaya ya Kati,
Jimbo la Uzini Kichama pamoja na kukabidhi pia mipira kwa ajili ya Timu
za Skuli 12 zilizomo ndani ya Jimbo la Uzini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/6/2013.
Post a Comment