Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma. |
Itakumbukwa tarehe 16/06/2013 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa baadhi ya kata nchini. Uchaguzi huo umefanyika kwenye kata ishirini na mbili (22) kati ya kata ishirini na sita (26) zilizotangazwa kufanya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi wazi.
Matokeo tuliyoyapata toka
kwenye maeneo yaliyofanya uchaguzi yanaonyesha kuwa kati ya kata 22 zilizofanya
uchaguzi CCM tumeshinda kata 16 sawa na asilimia 72.72% na wenzetu wamechukua
kata 6 zilizobaki sawa na asilimia 27.28%.
Tunawashukuru sana kote
walikoonyesha imani yao kubwa kwa Chama chetu kwa kutupa dhamana ya kuendelea
kuwatumikia. CCM inawaahidi utumishi uliotukuka. Hata wale 27.28% walioamua
kuwajaribu wenzetu, tunawatakia kila lakheri, kwani wametumia haki yao ya
kidemokrasia kuchagua wanaodhani watawasaidia kufikia malengo yao ya
kimaendeleo. Uchaguzi kwenye kata hizi zote umeisha sasa tuwatumikie
wananchi.
CCM tunalaani tukio hilo la
mlipuko wa bomu na matukio yanayofanana na hayo katika nchi yetu. Tunawapa pole
wale wote walioathirika na tukio hilo. Ni vizuri serikali ikalichunguza swala
hili kwa kutumia muda mfupi na kuhakikisha waliohusika wanapatikana na
kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Pamoja na kulaani na kuitaka
serikali kukomesha vitendo hivi nchini, ni wakati muafaka kwa vyama vya siasa
nchini kujitazama upya kwani kuna kila dalili kuwa tukio hili kama
alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mhe. Mbowe Mwenyekiti wa Chadema
Taifa kuwa ni la kupangwa, inawezekana limepangwa na Chadema
wenyewe.
Hali ya kisiasa jijini Arusha kuelekea uchaguzi
huo ilikuwa wazi kuwa wana Arusha walishaamua kuzirudisha kata hizo nne kwa CCM,
hasa baada ya kuchoshwa na maandamano na vurugu za kila siku jijini Arusha.
Aidha kauli za kukata tamaa za viongozi wa Chadema na vitendo vyao ni dalili
tosha kuwa tukio hili lilipangwa na Chadema wenyewe.
CCM tunaendelea kusisitiza na
kulaani juhudi za wenzetu kujaribu kujenga umaarufu wa chama chao juu ya damu za
Watanzania. Juhudi hizi zinapaswa kulaaniwa na wazalendo wote ndani na nje ya
nchi. Tukumbuke asiyekubali kushindwa, si mshindani. Si busara wala uungwana na
ni kinyume na utu kutumia majanga ya kutengeneza kama mtaji wa
kisiasa.
Lakini CCM tunalaani pia kitendo cha viongozi
wa Chadema kujaribu kutumia baadhi ya misiba na majeruhi wa tukio hili kisiasa
na mwisho wa siku kwenda kuwatelekeza hospitali baadhi yao baada ya kuwaahidi
kubeba gharama zote za matibabu na mazishi.Tunaipongeza serikali kwa kuingilia
kati na kuwasaidia waathirika hawa na kuhakikisha wanapata huduma
inayostahili.
CCM inarudia kueleza
masikitiko yake kwa waathirika wa tukio hili la kinyama na kikatili
lisilostahili kuvumiliwa hata kidogo. Kama Chama tumeguswa sana na tukio hili
pamoja na kulilaani, tunawasihi watanzania tushindane na kutofautiana bila
kupigana na kuvunja tunu ya nchi yetu ya amani na utulivu. Katika demokrasia ya
vyama vingi swala la kuvumiliana ni swala la msingi sana katika kufikia ukomavu
wa demokrasia hiyo.
Imetolewa;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi.
17/06/2013
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Ideology and Publicity
Secretary
Post a Comment