MWANAMKE mkazi wa kijiji cha Ikandamoyo,
wilayani Katavi, Veronica Saleh ‘Mama Kaela’ (50), amefanya uamuzi adimu wa
kuolewa na wanaume wawili ambao anaishi nao kijijini
hapo.
Kijiji hicho kipo umbali wa takribani
kilometa 30 kutoka mjini hapa katika Jimbo la Katavi linalowakilishwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na ndoa hiyo iliyowezeshwa na mume
mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo, imeelezwa kuwa mwanamke huyo ndiye
‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya miaka saba sasa, huku akiwa na amri kuu
katika nyumba, kama ilivyo katika ndoa za
kawaida.
Wanaume hao ni Paulo Sabuni ‘Baba Kaela’
(60) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (45) ambaye ni mume
mdogo.
Taarifa za kuwapo kwa ndoa hiyo ya aina
yake, ziliifikia Globu ya Jamii na kufanyiwa uchunguzi kwa zaidi ya wiki tatu,
na hatimaye katikati ya wiki hii, wahusika walikubali wao wenyewe kuzungumzia
suala hilo. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa
msemaji wa familia hiyo, yeye na mumewe mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24
iliyopita, wakitoka kijiji cha Usumbwa mpakani mwa Chunya, Mbeya na
Tabora.
Wakiwa kijijini hapo mume wake aliendelea
kufanya kazi ya ukulima wakati yeye mama (Veronica), pamoja na kilimo
hujihusisha na upishi na uuzaji wa pombe ya kienyeji iitwayo kayoga.
Mwanamke huyo ambaye amesema ana watoto
wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16 (ambaye ameolewa) na wengine wawili wa
kiume, mmoja akisoma darasa la sita na mdogo ana miaka saba, amesema hana shida
na waume wake.
Ingawa wanandoa hao walizungumza kwa
hadhari, majirani walikiri kuwa mwanamke huyo anaishi na wanaume hao wawili kwa
amani na kwamba mwanamke huyo ndiye mwenye sauti na si waume zake.
“Si siri tena sasa, tumeshawazoea, kwani
wanaishi kwa amani ila yule mume mdogo anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na
marehemu baba yake, lakini anashinda kwa mume mkubwa, ambapo inajulikana
kijijini hapa kuwa ni nyumba kubwa. “Basi pale ni mambo yote, kula na kunywa,
mama huyu amewapangia zamu wanaume hao kama afanyavyo mume mwenye wake
wengi.
Ama kweli ukistaajabu ya Musa utaona ya
Firauni,” alisema mkazi mmoja kwa masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini.
Ilielezwa, kwamba wanaume hao wana akili timamu na hawatumii kilevi cha pombe
kama ilivyo kwa mke wao.
Hata hivyo, mume mkubwa anapewa sifa za
upole tofauti na mume mdogo anayetajwa kuwa mkorofi kiasi cha mara kadhaa
kumchapa makofi mkewe anapomuudhi.
Majirani wanadai kwamba Mama Kaela na
mumewe Paulo, walipofika kijijini hapo, walipokewa na kuishi maisha ya kawaida,
lakini baadaye mama huyo alianza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Arcado, ambaye
naye alilazimika kuachana na mkewe wa ndoa anayefahamika kijijini hapo kwa jina
la Mama Pere.
Ilielezwa na mashuhuda hao kwamba mume
mkubwa alipobaini uhusiano huo, alikuja juu, lakini mwanamke huyo inadaiwa
alimweleza mumewe huyo, atake asitake lazima wataishi wawili, vinginevyo
ataachana naye, ndipo mume mkubwa alipokubali kuishi na mume mwenza.
Katika maisha ya kawaida katika familia
hiyo, inaelezwa kwamba katika baadhi ya siku ikitokea kuwa mama huyo amechoka
kupika, mume mdogo huchukua jukumu la kupika na kumwandalia chakula na maji ya
kuoga mume mkubwa.
“Lakini mara nyingi kwa mfano, ikiwa ni
zamu ya mama huyo kulala kwa mumewe mkubwa, basi humfulia nguo zake kisha
anakwenda kwa mumewe mdogo nako anamfulia
nguo.
MICHUZI BLOG
Post a Comment