Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani
Athumani
------------------------------------------
Na Gordon Kalulunga,
Mbeya
MKOA wa Mbeya ukiwa ni moja ya mikoa inayoongoza
kwa migogoro na kesi za ardhi, imefikia hatua sasa wananchi wameanza kuviziana
na kuuana.
Mkulima wa Kijiji cha Suma wilayani Rungwe Saita
Mboma(65), amefariki dunia baada ya kuvamiwa usiku nyumbani kwake na
kukatwakatwa na mapanga.
Taarifa ya Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya
iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari leo na kusainiwa na kamanda wa polisi
Diwani Athumani, imesema tukio hilo lilitokea Juni 22, mwaka huu kijijini hapo
na kukutwa na mauti Juni 24, mwaka huu.
‘Kabla hajapatwa na mauti alikimbizwa katika
hospitali ya Makandana wilayani humo kwa ajili ya matibabu ambapo taarifa
zinasema kuwa alikuwa akiishi peke yake na alivamiwa akiwa amelala na chanzo ni
mzozo wa muda mrefu wa mashamba’’ imeeleza taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa watuhumiwa wa tukio
hilo wamekamatwa ambao ni Salum Mwambona(45) na Feda Busila ambao wote ni wakazi
wa kijiji cha Itagata na taratibu za kuwafikisha mahakamani
zinafanywa.
Wakati huo huo, ajali za barabarani zimegeuka
janga la mkoa wa Mbeya ambapo hazipiti siku Nne bila kupoteza maisha ya
watanzania au kupata ulemavu wa kudumu.
Katika mwendelezo wa ajali hizo, askari Polisi wa
kikosi cha FFU Jijini Mbeya, amefariki papo hapo baada ya kugongwa na gari eneo
ya barabara ya Benki kuu Jijini hapa.
Taarifa polisi, imesema kuwa ajali
hiyo ilitokea Juni 23 mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema kuwa gari na dereva
asiyefahamika, liligonga gari T.741 BXU aina ya March lililokuwa limeegeshwa
eneo la hilo kisha kumgonga mtembea kwa miguu askari Polisi aitwaye
EX.G 9386 PC Patrick(23) na kusababisha kifo chake papo
hapo.
‘’Chanzo kinachunguzwa. Dereva alikimbia na gari
mara baada ya tukio na mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Dodoma kwa ajili
ya mazishi na yeyote mwenye taarifa za alipo dereva huyo na gari atoe taarifa
kwenye mamlaka husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake’’ imesema taarifa
hiyo.
Mbali na ajali hiyo, jana Juni 25, mwaka huu,
ajali nyingine imesababisha kifo cha Vedasto Emmanuel(20) na majeruhi kwa watu
watano eneo la Njia panda Ilomba Jijini Mbeya.
Watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Lusajo
John(22), Yohana Daud(20), Hussein Mbilinyi(20), ambao wamelazwa hospitali ya
rufaa ya Mbeya na mwingine ni Andrew Daud(20).
Post a Comment