VUGUVUGU
la Uchaguzi Mkuu wa 2015 linazidi kupamba moto ambapo juzi aliyekuwa
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, ameomba CCM itoe ruhusa mapema kwa
wanaowania urais kuanza kutangaza nia lakini bila kukampeni.
Sumaye ambaye alipata kugombea urais mwaka 2005, alionya kuwa kama
CCM haitaruhusu wagombea kutangaza nia leo, yanayofanyika chini chini ni
mabaya zaidi.
Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 juzi, Sumaye mbali na
kuitaka CCM kuruhusu wanachama wake kuan
za kutangaza nia ya kugombea
mapema, pia alielezea athari za muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa
na Rasimu ya Katiba mpya na mfumo mpya wa kusoma Bajeti ya Serikali
bungeni.
Urais 2015
“Mimi Sumaye nikisema sasa nitagombea urais mwaka 2015 hakuna ubaya
kwa kuwa Watanzania, watapata muda kunichambua na mpaka miaka miwili
ikifika wakati wa kugombea, watakuwa wananifahamu,” alisema Sumaye.
Alihadharisha kuwa kama CCM itaendelea kukataza watu kutangaza nia
mapema, wataanza kupita chini chini na madhara yake ni makubwa kuliko
kuanza kutangaza nia mapema.
Kwa mujibu wa Sumaye, alisoma katika vyombo vya habari vikimkariri
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiruhusu wanaotaka kugombea
urais, waanze kujitangaza lakini wasifanye vurugu, akaona ni hatua
nzuri.
Lakini muda mfupi baadaye, alisoma vyombo vya habari vikimkariri
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape
Nnauye, akisema watakaoanza kujitangaza chama kitawaengua.
“Sasa sina hakika na taarifa hizi za vyombo vya habari kwa kuwa
katika matamshi hayo yote mimi sikuwepo... natii msimamo wa chama
changu, ingawa binafsi nadhani ni vema tutangaze mapema lakini tusifanye
kampeni,” alisema.
Katiba ya mapambano
Akizungumzia Rasimu ya Katiba mpya, Sumaye alisema mapendekezo ya
Serikali tatu katika Rasimu hiyo, hata yeye aliona mapema kuwa
hayaepukiki, lakini athari yake ni kujenga mapambano makubwa kati ya
serikali hizo.
Alipendekeza wakati wa kujadili Rasimu, Watanzania watoe maoni ya
namna ya kupunguza mapambano hayo ambayo yanaweza kuwa magumu kuliko
wakati huu wa serikali mbili.
Alitoa mfano wa mapambano yaliyopo wakati huu wa serikali mbili
kwamba yalisababisha Zanzibar ikaanza kudai Wimbo wa Taifa, Rais wa
Zanzibar kupigiwa mizinga ambayo ilianza 19, sasa ni 21.
Mapambano mengine ni Zanzibar kudai kuwa Tanzania Bara inafaidika kwa
kuwa Rais wa Jamhuri anasimamia mambo ya Muungano na ya Bara, wakati
Bara inaona Muungano unaibeba Zanzibar.
“Kama mapambano haya hatujayaondoa wakati huu wa serikali mbili,
katika serikali tatu mapambano ya Zanzibar na Bara ambayo watu wanaweza
kuiita Tanganyika, yatakuwa makubwa zaidi na pengine mabaya,” alisema
Sumaye.
Katika mfumo wa serikali tatu, Sumaye alihadharisha kwamba mapambano
yataanzia katika mgawanyo wa rasilimali, wakati wa kugawa kodi za
Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Bara.
Alihadharisha kuwa kuna uwezekano wa kutokea mapambano kati ya
Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanzania Bara katika mgawanyo wa
rasilimali na akaongeza kwamba kwa kuwa Serikali hizo mbili hazitakuwa
na tofauti kubwa, mapambano hayo yatakuwa mabaya.
Mapambano mengine alisema yataanzia katika madaraka, ambayo alitoa
mfano wa madai ya Zanzibar ya wakati wa serikali mbili, kwamba wakati wa
serikali tatu, Bara nayo italeta madai yake.
Katika utendaji, Sumaye alisema pia kutakuwa na mapambano, kwa kuwa
kutakuwa na marais watatu, makatibu wakuu viongozi watatu na makatibu
wakuu wengine.
“Kwa sasa makatibu wakuu hawaingiliani, lakini katika serikali tatu,
watavutana,” alihadharisha. Utaratibu mpya wa Bajeti Akizungumzia
utaratibu mpya wa bajeti ya Serikali ambao wabunge wanaanza kujadili
bajeti za wizara na kumaliza na Bajeti ya Serikali, Sumaye alisema
utaratibu huo ni mbovu.
Kwa mujibu wa Sumaye, kwa utaratibu wa sasa Waziri akibanwa,
atakubali kuongeza bajeti na hivyo atalazimika kurudi kwa wananchi,
kutoza kodi zaidi ili apate hizo fedha.
Alisifu utaratibu wa zamani wa kuanza na Bajeti ya Serikali, kwa kuwa
ilizuia bajeti kuvurugwa na wabunge walikuwa na fursa ya kubadili
mafungu tu na si kuongeza bajeti.
“Kwa sasa wabunge wanaweza kutaka fedha nje ya mfuko wa bajeti, sasa
Serikali ifanyeje? Waziri ataongeza kodi mpaka atamwumiza mlipa kodi,”
alisema Sumaye.
CHANZO HABARILEO.
Post a Comment