|
Arusha. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema bomu lililolipuliwa katika mkutano wa Chadema ni la kijeshi na limetengenezwa China.
Akizungumza mjini hapa jana, Pinda alisema
uchunguzi unaendelea kujua bomu hilo limefikaje kwenye mikono ya
waliohusika kwani uzoefu unaonyesha kuwa hutumiwa na wanajeshi kujihami
wakiwa katika makabiliano na maadui vitani.
“Ingawa uchunguzi unaendelea, lakini inawezekana
bomu hilo limeingizwa nchini na wahalifu wasiojulikana kupitia njia za
panya za mipakani,” alisema Pinda.
Serikali kusimamia mazishi
Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kwamba itasimamia mazishi ya watu waliopoteza maisha kutokana na shambulio hilo.
Hatua hiyo imekuja huku Chadema nacho kikiwa
kimetangaza kushughulikia mazishi ya wananchi hao kwa kuwa walifariki
katika shambulio lililotokea kwenye mkutano wao.
Waziri Mkuu, jana alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Magessa Mulongo kusimamia shughuli zote za misiba hiyo, agizo
ambalo wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ni kama kuipokonya
Chadema dhamana ya kusimamia shughuli za mazishi hayo.
Juzi jioni, Mbowe aliwaambia wananchi na wafuasi
wa Chadema katika Viwanja vya Soweto kuwa chama chake kitagharimia na
kusimamia shughuli zote za kuaga, kusafirisha pamoja na mazishi ya
waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Chama hicho tayari kilishafunga mahema katika
Viwanja vya Soweto kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini uongozi wa Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), kilizuia kuendelea kwa
shughuli hiyo hali iliyosababisha machafuko.
|
on Wednesday, June 19, 2013
Post a Comment