01
Mwanachi wa Zanzibar akichangia Damu katika madhimisho ya wachangia Damu Duniani kwenye Benki ya Damu salama Sebleni.
03
Waziri wa Afya Juma Duni Haji akiwataka wananchi kuchangia Damu katika Benki ya Damu salama katika madhimisho ya wachangia Damu Duniani.
04
Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Cheti maalum cha kuthamini michango yao, muakilishi wa KMKM Dokta Foum Ali Abdalla, huko Benki ya Damu Sebleni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
02
Wafanyakazi wa Benki ya Damu Zanzibar, wakifutilia hutuba ya Makamo wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Iddi katika madhimisho ya wachangia Damu Duniani Sebleni. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.)
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar
Serikali ya Zanzibar imeahidi kuzimaliza changamoto zote zinazokikabili Kitengo cha Damu Salama ili kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wachangiaji Damu Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Benki ya Damu Zanzibar huko Sebleni, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, amesema serikali inafahamu umuhimu wa kitengo hicho kwa maisha ya wananchi.
Alisema, ni ukweli usiofichika kuwa, wananchi wanaojitolea kuchangia damu kwa hiyari, wana mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi wenzao, ambao hupata matatizo mbalimbali yanayowalazimu kuongezewa damu.
Balozi Seif alieleza kuwa, kuchangia damu ni zawadi ya maisha, kwani wanaoihitaji wakiwemo wajawazito wanaojifungua kwa upasuaji, majeruhi wa ajali na watoto wenye upungufu wa damu, hunufaika kwa kuwepo akiba ya damu ya kutosha.
Makamu wa Pili wa Rais aliipongeza Jumuiya ya Wachangiaji Damu kwa Hiyari Zanzibar (JUWADAHIZ), kwa juhudi kubwa ilizofanya kukiimarisha kitengo cha damu salama, na kuitaka kuzidi kuwashajiisha vijana wengine wajiunge nayo kwa wingi.
Aidha aliwasihi vijana kujitokeza kwa wingi katika uchangiaji damu, ili kuzifanya huduma hizo kuwa endelevu, na kuwataka kutokuwa na woga kwani kwa kufanya hivyo pia, wataweza kujua afya zao, na kama wana matatizo yoyote yatashughulikiwa mapema
Kwa upande mwengine, alisema kuwepo kwa Benki ya Damu, kunasaidia sana kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI, kwani kusingekuwepo wachangiaji damu, kasi ya maradhi hayo ingeongezeka zaidi.
Alichukua fursa hiyo kwa niaba ya serikali, kuwapongeza washirika wa maendeleo, Benki ya Watu wa Zanzibar pamoja na Mfuko wa Hifathi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), kwa kutoa misaada mbalimbali ili kukiendeleza kitengo hicho.
Hata hivyo, aliwataka madereva wa vyombo vya barabarani, kuwa waangalifu wakati wakiendesha, na kuacha uzembe unaosababisha ajali nyingi zinazopoteza maisha ya watu na kuwaacha wengine na vilema vya maisha.
Mapema, Waziri wa Afya Juma Duni Haji, alisema wizara yake iko makini kwa kushirikiana na kitengo cha damu, katika kupiga vita tabia ya kuwauzia damu watu wanaohitaji kutokana na matatizo mbalimbali, na kuwachukulia hatua kali watakaobainika wakifanya biashara hiyo.
Akifafanua juu ya umuhimu wa damu kwa binadamu, Duni alisema mtu anapokuwa mzima, hawezi kujua thamani ya damu, bali huijua pale anapopata matatizo.
“Lazima wananchi wa Zanzibar wahamasike kujiunga na Jumuiya ya Wachangiaji Damu kwa Hiyari ili benki yetu iwe na akiba ya kutosha kwani matatizo hayana miadi, humtokezea mtu wakati wowote”, alisisitiza Duni.
Naye Meneja wa Kitengo cha Damu Salama Mwanakheir Ahmed, alisema ili mpango huo uwe endelevu, ni lazima kuwepo na idadi kubwa ya wachangiaji damu, kwa kuzingatia kuwa mahitaji yanaongezeka kila uchao.
Jumuiya ya Wachangiaji Damu Zanzibar, ina wanachama 850 wanaume na wanawake Unguja na Pemba, na pia imeanzisha klabu ndogo ndogo zipatazo 63 ili kurahisisha upatikanaji wa damu.
Kati ya klabu hizo, 43 ziko Unguja na 20 kisiwani Pemba.