Na Saleh Ally
Kiungo nyota wa zamani Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ na beki Juma Nyosso wataanza maisha
mjini Tanga kwa kuishi kwenye nyumba ambayo imewekewa ‘AC’ au kiyoyozi kwa muda
wote watakaokuwa mjini Tanga.
Uongozi wa
Coastal Union, umesema umeamua kukodisha hoteli moja maarufu ya mjini humo
ambayo iko kwenye ufukwe na kuifanyia ukarabati wa hali ya juu.
Mdhamini
Mkuu wa Coastal Union, Mohammed Bin Slum amesema, kila chumba katika hoteli
hiyo itakuwa na kiyoyozi na ndani yake kutakuwa na ukumbi maalum wenye michezo
mbalimbali.
“Wachezaji
wataishi katika hoteli hiyo ya nyota tano na ukarabati uko katika hatua za
mwisho. Tumeamua pia kuwawekea michezo mbalimbali kama pool, tenisi na plays
station ili kuwafanya watulie wanapokuwa pale,” alisema Bin Slum.
“Lakini
kutakuwa na tv sehemu maalum kwa ajili ya wao kupata nafasi ya kuona mechi
mbalimbali zikiwemo zile za kimataifa.
Lengo ni kuwafanya wachezaji wawe katika hali ya utulivu na vizuri zaidi
makocha na benchi la ufundi wataishi hapo.”
Alipoulizwa
sababu ya kubadili mfumo wa misimu iliyopita ambayo baadhi ya wachezaji
walikuwa wamepangiwa nyumba, alisema:
“Mwisho
tumeona si sahihi, maana kuna baadhi ya wachezaji hawakuwa waaminifu. Sisi
tuliwaamini kama professional lakini wao wakatuangusha na wengi wakatoroka
usiku kwenda kufanya starehe na mambo ya wanawake. Sasa tumeamua kutumia mfumo
mwingine.”
Boban na
Nyosso wamekuwa gumzo kubwa baada ya kuamua kujiunga na Coastal Union kwa ajili
ya msimu ujao baada ya kutokuwa na maelewano mazuri na uongozi wa Simba.
Boban
alijiunga na Coastal Union baada ya uongozi wa Simba ‘kumkaushia’ wakati Nyosso
aliamua kuvunja mkataba na kutua zake kwa Wagosi wa Kaya.
Post a Comment