HOTUBA
YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA TAMASHA LA MATUMAINI, UWANJA WA TAIFA DAR ES
SALAAM, TAREHE 07 JULAI, 2013
Ndugu Wananchi;
Nakupongeza
sana ndugu Erick Shigongo kwa kuandaa tamasha hili adhimu lenye
mchanganyiko wa mambo mengi. Bahati nzuri mambo yote ni mazuri na
yanayalifanyia taifa letu mambo mema. Sala ya pamoja kuliombea taifa,
burudani mbalimbali zikiwemo za muziki, mchezo wa ngumi na mpira wa
miguu.
Pengine
faida kubwa zaidi ya Tamasha lenyewe hili ni kujenga moyo wa upendo,
umoja, ushirikiano na moyo wa uzalendo miongoni mwa Watanzania wa marika
yote: watoto, watu wazima na wazee. Miongoni mwa watu wa makabila yote,
rangi zote, dini zote na miongoni mwa wafuasi wa vyama vyote vya siasa.
Katika kipindi hiki ambacho
maadui wa umoja, amani na utulivu wa nchi yetu wanahangaika usiku na
mchana kuleta mifarakano miongoni mwa Watanzania, matukio kama Tamsha
hili ndilo jibu zuri kwao. Kupitia Tamasha kama hili tunawajibu kuwa
Watanzania hatutaki, hatukubali na wala hatudanganyiki. Tuwapelekee
ujumbe huo bila kumung’unya maneno kuwa njama zao zimeshindwa na kamwe
hazitafanikiwa.
Lakini, tamasha hili pia
lipeleke ujumbe kwa wanasiasa na wafuasi wao kuwa kutafuta umaarufu,
kuungwa mkono au ushindi kwa kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania
kwa misingi ya dini zao, rangi zao, na maeneo watokayo nako
hakutawasaidia. Walishindwa wakoloni kwa sera yao ya wagawe uwatawale,
hataweza mswahili. Isitoshe ni kutenda dhambi kubwa na kutowatendea haki
Watanzania, Mungu wao, dini zao na vyama vyao vya siasa kuingiza dini
katika siasa au siasa katika dini. Kiongozi wa siasa anayesema dini yetu
ni hii au kiongozi wa dini anayesema Chama chetu ni hiki wote ni
wababaishaji. Wanasema mambo ambayo hayana uhusiano wo wote na dini.
Kiongozi wa dini huyo awe mkweli tu kwamba, ni mwanachama au mpenzi wa
Chama cha siasa aliyeamua kutumia nafasi yake ya uongozi wa dini au
uumini wake kuendeleza maslahi ya Chama chake. Hakuna lolote la dini
hapo na wala hakuna kitabu kitakatifu cha dini yoyote kinachotaja Chama
cha siasa cha kufuata.
Kiongozi wa siasa anayetumia
dini kujenga Chama chake amefilisika hoja za kisiasa. Isitoshe Sheria ya
Usajili wa Vyama iko wazi. Inazuia kutumia udini, ukabila na aina zote
za ubaguzi. Watu hawa wamegubikwa na tamaa ya madaraka iliyovuka mipaka
ya utu. Sijui kama watu hawa hawatambui athari zake. Tunaweza kufika
siku makanisa na misikiti ikagawanyika kwa upenzi na ufuasi wa vyama vya
siasa. Tutazikwaza dini zetu na nchi yetu kuiweka mahala pabaya.
Tuwaache wanasiasa na
wanachama wagawanyike kwa vyama vyao wanavyovipenda lakini makanisa na
misikiti pawe mahali pa kuwaunganisha. Mwenyezi Mungu awe ni
muunganishaji wao. Lakini tukiendelea na mikakati ninayoiona na kuisikia
inaendelea hata katika nyumba za ibada, viongozi wa dini watashindwa
kuwaunganisha waumini wao. Badala ya watu kutambuana kama Waislaimu au
Wakristo wataanza kujuana kwa vyama vya siasa. Ni hatari kubwa kwa dini
kwani upenzi wa watu kwa vyama vya siasa ni vitu vinavyobadilika
kulingana na sera, matukio na mazingira. Hivi tunataka na imani ya watu
kwa dini iwe inabadilika na mazingira?
Tuyalinde mambo
yanayotuunganisha ili yadumu. Tusiyaendekeze mambo yanayotugawa. Pale
ambapo siasa zinagawanisha, dini, michezo na mengineyo yanayowaunganisha
yatekelezwe kwani yanaweza kusaidia kupunguza uhasama na yanaweza
kusaidia kuponya. Zitto Kabwe na William Ngeleja wako vyama viwili
vinavyoshindana katika majukwaa ya siasa, lakini leo watacheza upande
mmoja wa Wabunge wa Simba. Halima Mdee, Grace Kiwelu, Mohamed Misinga
wao ni viongozi wa Yanga Bungeni. Mambo yanayotuunganisha tuyape
kipaumbele kusisitiza umoja wetu, kujenga upendo na kupunguza makali ya
tofauti zetu.
Ndugu Shigongo wa Global
Publishers nakupongeza sana kwa kufanya jambo linaloponya jamii. Matukio
kama haya yanatakiwa yawe mengi zaidi nchini kwani yana manufaa makubwa
kwa nchi yetu na watu wake. Sisi katika Serikali tunaunga mkono.
Yaendelezeni na yadumisheni.
Nakushukuru pia kwa uamuzi
wako wa busara wa kutumia asilimia 20 ya pesa zinazokusanywa kusaidia
ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule nane za sekondari katika
mikoa ya Manyara, Tanga, Dodoma, Lindi, Ruvuma, Mara, Mwanza na Kigoma.
Ni jambo jema sana. Asante sana.
Kwa ndugu zangu Wabunge,
wasanii wa muziki na filamu na wanamichezo wengine waliojitolea
kutuburudisha leo nawapongeza na kuwatakia kila heri. Tumekuja
kuwashuhudia na kuburudika nanyi. Naomba mtuburudishe na kuwaonyesha
vijana kuwa ujuzi hauzeeki.
Kwa mara nyingine nashukuru kualikwa.
Asanteni sana.
Post a Comment