Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

JWTZ KUONGEZA WANAJESHI ZAIDI WA KULINDA AMANI DARFUR NCHINI SUDAN.

 

JWTZ kuongeza nguvu zaidi Darfur 

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), linatarajia kuongeza nguvu ya kujilinda, wakati wa kulinda amani katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, ili kujikinga na mashambulizi kama la juzi, ambalo lilisababisha askari wake saba kupoteza maisha.
Msemaji wa JWTZ Kanali Kapambala Mgawe, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumzia shambulio hilo, lililosababisha pia majeruhi wengine 14.

Kauli hiyo imetolewa wakati Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete akiungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapigan
aji wa JWTZ na familia za wafiwa, kuomboleza vifo vya vijana hao hodari wa Tanzania.
Nguvu zaidi

Kanali Mgawe alisema mawasiliano yanafanyika kati JWTZ na Umoja wa Mataifa (UN), kuhusu uwezekano wa kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi, wakati askari wa Tanzania wanapokabiliana na mashambulizi hayo.

“Kama inavyojulikana, kikosi chetu kipo kule kulinda amani kwa mujibu wa makubaliano ya Umoja wa Mataifa (UN) Sura ya Sita, ambayo yanataka kusitumike nguvu sana, sasa tunataka tutumie Sura ya Saba inayotoa fursa ya kuongeza uwezo wa kujilinda.
“Mawasiliano yanafanyika kati yetu na UN kuhusu uwezekano wa kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi wakati wa mashambulizi hayo,” alisema Kanali Mgawe.

Hali ilivyokuwa Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao wanaounda kikosi cha wanajeshi 875, walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja.

Walipatwa na mkasa huo saa tatu asubuhi juzi Jumamosi, wakati wakisindikiza msafara wa waangalizi wa amani kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyara, Darfur na ghafla walishambuliwa na kikundi cha waasi wa Sudan.

Kanali Mgawe alisema kutokana na majukumu ya kikosi hicho na makubaliano ya UN Sura ya Sita, haikuwa rahisi kufikiria kuwa wangekutana na shambulizi hilo, kwa kuwa hata eneo hilo halina historia ya matukio kama hayo.

Taarifa ya Msemaji wa Vikosi vya UN, Chris Cycmanick iliyotolewa juzi jioni, ilieleza kuwa shambulio hilo lilifanywa na kundi kubwa la watu waliokuwa na silaha nzito za kivita, ikiwemo mabomu ya kutupwa kwa roketi.

Cycmanick alisema shambulio hilo, lilitokea kilometa 20 kutoka makao makuu ya kikosi hicho, Khor Abeche na Kikosi cha Uokoaji kilifika baadaye kunusuru majeruhi 14, akiwemo askari Polisi mmoja.

Miili ya marehemu hao na majeruhi, waliondolewa na kupelekwa Nyara kwenye Hospitali Kuu ya eneo la Operesheni, kuhifadhi miili na kutoa matibabu kwa majeruhi.

JWTZ kwa sasa inawasiliana na familia za marehemu, kuhusu taratibu za mazishi na UN kwa ajili ya taratibu za matibabu kwa askari wote, waliojeruhiwa katika eneo la tukio.

Kanali Mgawe aliahidi JWTZ itaendelea kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kadri watakavyozipata, baada ya ujumbe wa Tanzania uliotumwa Darfur kuwasili nchini humo.

JK awalilia
Rais Kikwete ameelezea kushtushwa na kuhuzunishwa na mauaji hayo na ametuma salamu za rambirambi za moyoni mwake kwa JWTZ kwa familia za wafiwa wote.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange na familia za wafiwa, Rais Kikwete alisema: 
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshituko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kutokana na vifo vya vijana wetu hao, ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa, ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waasi.

”Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu, niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa. Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao.”

Katika salamu hizo, Rais Kikwete alisema: “Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza vijana wetu hawa.

Kupitia kwao, natuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapiganaji wote wa Jeshi letu kwa kupotelewa na wenzao.

Kwa familia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo, Rais Kikwete alisema uchungu wao ni uchungu wake pia na wa Watanzania wote, na kumuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.

“Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu. Amina.”

Kwa walioumia, Rais Kikwete alisema anawaombea wale walioumia katika tukio hilo, wapone haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya UN.

“Naungana pia na Watanzania wenzangu katika kuwapa pole nyingi walioumia katika tukio hilo, tukiwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea na shughuli zao za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa,” alisema.

Kauli ya UN.
Katika taarifa ya UN iliyotolewa na Cycmanick, Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon amesema karibu nchi 40 zimekuwa zikichangia wanajeshi au polisi kwa ajili ya kulinda amani.
Ban amesema shambulio hilo, ambalo ni la tatu katika muda wa wiki tatu zilizopita, ni la kigaidi na ametoa rambirambi zake kwa familia za wafiwa.

“Natarajia Serikali ya Sudani litachukua hatua kali kuwasaka wahusika na kuwafikisha katika mkono wa haki,” taarifa hiyo ilieleza. CHANZO HABARILEO
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top